Thursday, February 14, 2013

LIBYA YAKATAA KUMKABIDHI SENUSSI ICC

Serikali ya Libya imepinga ombi la kumkabidhi Abdullah al-Senussi aliyekuwa mkuu wa shirika la ujasusi la utawala uliong’olewa madarakani wa Muammar Gaddafi kwenye Mahakama ya Kimataifa ya Jinai (ICC).
Vyombo vya Sheria vya Libya vimeeleza kuwa vina uwezo wa kusikiliza kesi inayowakabili viongozi wa zamani wa nchi hiyo na kwamba havihitaji msaada wa mahakama ya ICC. Mahakama ya ICC iliyoko The Hague nchini Uholanzi, jana iliitaka serikali ya Libya imkabidhi Abdullah al-Senussi ili imfungulie mashtaka kwenye mahakama hiyo ya kimataifa. Al-Senussi anatuhumiwa kuwa aliuwa wanamapinduzi waliokuwa wakipinga utawala wa Gaddafi.
Mahakama ya ICC imetangaza kuwa, iwapo Libya haitamkabidhi al-Senussi suala hilo litawasilishwa kwenye Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa. Mkuu wa zamani wa shirika la ujasusi la Libya alitiwa mbaroni mwanzoni mwa mwaka 2012 nchini Mauritania.

No comments:

Post a Comment

TUPE MAWAZO YAKO