Wanamgambo wa Al-Shabab wanaripotiwa kuuteka mji wa Hudur wa kusini mwa Somalia. Mashuhuda wanasema kuwa, mji wa Hudur ulioko katika mkoa wa Bakool kusini mwa Somalia sasa unadhibitiwa tena na wanamgambo wa Al-Shabab baada ya vikosi vya Ethiopia kuondoka katika mji huo. Baadhi ya raia wamewaambia wanahabari kwamba, vikosi vya serikali ya Somalia na vile vya Ethiopia pamoja na raia wameondoka katika mji wa Hudur wakihofia usalama wa maisha yao. Tukio la kudhibitiwa tena mji wa Hudur linajiri mwezi mmoja tu baada ya vikosi vya kulinda amani vya Umoja wa Mataifa vikishirikiana na vikosi vya serikali ya Somalia kuudhibiti mji huo mwezi uliopita. Mji huo wa kiistratejia upo kilomita 190 kusini mwa Mogadishu mji mkuu wa Somalia. Kundi la wanamgambo wa Al-Shabab limeahidi kumuondoa madarakani Rais Hassan Sheikh Mohamud wa Somalia aliyechukua hatamu za uongozi wa nchi hiyo ya Pembe ya Afrika Septemba mwaka jana. Hivi karibuni Rais Hassan Sheikh Mohamud wa Somalia alisema kuwa yuko tayari kuwajumuisha wanachama wa kundi la Al-Shabab katika jeshi la taifa iwapo wataamua kuweka silaha chini na kujisalimisha kwa serikali.
No comments:
Post a Comment
TUPE MAWAZO YAKO