Sunday, March 03, 2013

IRAN KUWA NA NYUKLIA KWAPITISHWA NA NAM


Nchi zaidi ya 100 wanachama wa Harakati ya Nchi Zisizofungamana na Siasa za Upande Wowote (NAM) kwa mara nyingine tena zimeunga mkono miradi ya kuzalisha nishati ya nyuklia ya Iran. Ali Asghari Sultaniye mwakilishi wa Iran katika Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Nyuklia (IAEA) amesema kuwa uungaji mkono wa NAM kwa miradi ya nyukilia ya Iran ni miongoni mwa masuala yaliyojadiliwa na kupasishwa katika kikao cha jana cha mabalozi wa harakati ya NAM kilichofanyika mjini Vienna, Austria. Sultaniye amesema kuwa kupasishwa taarifa hiyo kumebeba ujumbe chanya zaidi ambapo wawakilishi wa harakati ya NAM katika wakala wa IAEA wameunga mkono matumizi ya nishati ya nyuklia kwa malengo ya amani kwa mujibu wa mkataba wa NPT sambamba na kuunga mkono miradi ya nyuklia ya Iran.
Hii si mara ya kwanza kwa harakati ya NAM kuunga mkono wazi wazi shughuli za kuzalisha nishati ya nyuklia za Iran. Katika taarifa yake kama hii iliyoitoa huko nyuma, Harakati ya Nchi Zisizofungamana na Siasa za Upande Wowote (NAM) pia iliwasilisha mapendekezo na ushauri kwa wakala wa IAEA na kutangaza kuwa inaunga mkono haki za kinyuklia za Iran. NAM pia ilitangaza uungaji mkono wake huo kwa miradi ya nyuklia ya Iran katika kikao cha wakuu wa harakati hiyo kilichofanyika mwaka jana mjini Tehran.  
Harakati ya NAM ilisisitiza kwenye taarifa hiyo juu ya udharura wa kuimarishwa hali ya kuaminiana katika utendaji wa kitaalamu na kusisitiza juu ya umuhimu wa kutoegemea upande wowote bodi ya wakala wa IAEA katika kutekeleza shughuli zake. NAM pia ilisisitiza juu ya haki ya kimsingi na ya wazi ya nchi zote ya kustawisha, kumiliki, kuzalisha na kutumia nishati ya nyuklia kwa malengo ya amani bila ya ubaguzi wowote na kwa mujibu wa sheria.
Taarifa ya hivi karibuni ya harakati ya NAM pia imepasishwa siku mbili kabla ya kufanyika kikao cha bodi ya magavana ya wakala wa IAEA huko Vienna, Austria ambako moja ya masuala yatakayojadiliwa kwenye kikao hicho ni ripoti ya Mkurugenzi Mkuu wa wakala huo Yukia Amano kuhusu Iran.
Harakati ya Nchi Zisizofungamana na Siasa za Upande Wowote inautambua wakala wa IAEA kuwa ndio taasisi pekee yenye mamlaka ya kushughulikia na kusimamia masuala ya nyuklia na ni kwa msingi huo  ndio maana NAM ikabainisha wasiwasi wake kuhusu mashinikizo au uingiliaji wa baadhi ya nchi katika utendaji wa IAEA unaoweza kuutia hatarini uwajibikaji na hadhi yake.
Suala liinalopewa umuhimu na nchi wanachama 120 wa harakati ya NAM ni kutimizwa kaulimbiu ya kimataifa ya kuwa na ulimwengu usio na silaha za nyuklia. NAM inasisitiza mara kwa mara katika taarifa zake kuwa suala la kupiga marufuku uenezaji wa silaha za nyuklia linaweza kupatiwa ufumbuzi kwa njia za kisiasa na kidiplomasia na kwamba hatua zilizochukua katika uwanja huo zinapaswa kufanyika kwa mujibu wa sheria za kimataifa, maazimio husika na hati ya Umoja wa Mataifa.

No comments:

Post a Comment

TUPE MAWAZO YAKO