Tuesday, March 19, 2013

JESHI LA UFARANSA NCHINI MALI LATUMIA SILAHA ZILIZOPIGWA MARUFUKU


Askari wa Ufaransa wametumia silaha zilizopigwa marufuku kimataifa katika mashambulizi yake ya kijeshi nchini Mali katika kukabiliana na makundi ya waasi wa kaskazini mwa nchi hiyo. Kundi la Ansaruddin la kaskazini mwa Mali limetoa taarifa likisema kuwa, jeshi la Ufaransa limetumia silaha zenye urani iliyohafifishwa kwa ajili ya kulipua mapango ya milima ya Ifoghas. Taarifa hiyo imesema kuwa jeshi la Ufaransa likishirikiana na lile la Mali limetia sumu katika visima vya maji vilivyo karibu na milima ya Ifoghas na kuzidisha kiwango cha joto katika eneo hilo kwa shabaha ya kuwatia kiu zaidi wapiganaji wa makundi ya upinzani.
Kamanda mmoja wa zamani wa kundi la Ansaruddin amethibitisha habari hiyo na kusema kuwa hatua hiyo ya jeshi la Ufaransa ni mbinu mpya inayotumiwa kwa shabaha ya kuzidisha mzingiro dhidi ya mamia ya wapiganaji waliokimbilia katika milima ya Ifoghas. Tarehe 11 Januari Ufaransa iliishambulia nchi ya Mali kwa uungaji mkono wa Marekani, Uingereza na Ujerumani kwa kisingizio cha kupambana na ugaidi na makundi eti yenye misimamo mikali. Hata hivyo baadhi ya wachambuzi wa mambo wanasema kuwa, lengo hgalisi la mashambulizi hayo ni kutaka kuhuisha satuwa na ushawishi wa Ufaransa na waitifaki wake katika eneo la magharibi na kaskazini mwa Afrika. Ufaransa bado inaendeleza mashambulizi hayo licha ya upinzani mkubwa wa fikra za waliowengi, vyama vya siasa na hata umwagaji damu mkubwa uliosababishwa na uvamizi huo.
Rais François Hollande wa Ufaransa jana alitoa taarifa akitangaza habari ya kuuawa askari wa tano wa nchi hiyo katika vita vya Mali. Kwa kutilia manani suala hilo wachambuzi wa mambo wanaashiria kushadidi mapigano huko kaskazini mwa Mali na kuongezeka mashambulizi ya waasi. Wanasisitiza  kuwa operesheni ya jeshi la Ufaransa katika eneo hilo imegonga mwamba. Wanasema huenda ni kwa sababu hiyo ndiyo maana Paris imeamua kutumia silaha zilizopigwa marufuku kimataifa kwa kuchea kushindwa huko kaskazini mwa Mali. Vyombo mbalimbali vya habari vya kieneo na kimataifa vinasema kuwa mbali na kutumia makumi ya ndege za kisasa za kivita, Ufaransa pia inatumia vikosi vya majeshi ya nchi kavu na silaha nzito na nyepesi katika vita vya umwagaji damu huko kaskazini mwa Mali. Waziri wa Ulinzi wa Ufaransa Jean - Yves le Drian amesema kuwa nchi yake imetuma askari elfu nne wa kikosi maalumu nchini Mali. Katika mashambulizi hayo Ufaransa inapewa misada ya kilojistiki ya Marekani, nchi za Ulaya na hata baadhi ya nchi za Kiafrika.
Nchi za Magharibi zimekuwa zikizishambulia nchi mbalimbali dunia kwa ajili ya kudhamini maslahi yao haramu kwa kutumia kisingizio cha kupambana na ugaidi. Kwa sasa bara Afrika ni miongoni mwa maeneo muhimu ya kiuchumi duniani yanayokodolewa macho na nchi za Ulaya. Kwa msingi huo nchi wakoloni wa zamani katika bara la Afrika zinatumia nyenzo za aina mbalimbali kwa shamaba ya kurejea tena barani Afrika. Mfano hai wa ukweli huo ni mashambulizi ya sasa ya jeshi la Ufaransa huko kaskazini mwa Mali, nchi inayosifika kwa kuwa na akiba kubwa ya maliasili ikiwa ni pamoja na utajiri wa madini ya urani na dhahabu.

No comments:

Post a Comment

TUPE MAWAZO YAKO