Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu wa kivita ya ICC iliyoko mjini The Hague nchini Uholanzi imesema haitamuondolea mashtaka yanayomkabili rais mteule wa Kenya, Uhuru Kenyatta. Kiongozi wa Mashtaka katika Mahakama hiyo Fatou Bensouda amesema kuwa suala lililoko kwa sasa ni lini Kenyatta atashtakiwa wala sio kama atafikishwa mahakamani au kufutiwa mashtaka yanayomkabili.
Bensouda amewaambia waandishi wa habari jijini Paris nchini Ufaransa kuwa ana ushahidi wa kutosha kumshtaki Kenyatta anayetuhumiwa kufadhili na kuchochea machafuko ya baada ya uchaguzi nchini Kenya mwaka 2007 mjini Nakuru na Naivasha. Mawakili wa Kenyatta mapema juma hili waliwaomba Majaji wa Mahakama hiyo kuirudisha kesi hiyo katika Mahakama ya kuthibitisha ikiwa mteja wao ana kesi ya kujibu kwa kile walichodai kuwa upande wa mashtaka umebadilisha mashtaka dhidi yake na pia mshukiwa mwenzake Francis Muthaura alifutiwa mashtaka yaliyokuwa yanamkabili.
Ikiwa Majaji wa Mahakama hiyo hawatairudisja kesi hiyo katika Mahakama ya kuthibitisha ikiwa Kenyatta ana kesi ya kujibu au la, na ikiwa ataapishwa kama rais wa Kenya atakuwa rais wa kwanza kuhudhuria vikao vya ICC tangu Mahakama hiyo ilipoanza kazi yake mwaka 2002.
Kesi ya Kenyatta ambaye alitangazwa kama rais mteule wa Kenya wiki moja iliyopita, inatarajiwa kuanza mwezi Julai mwaka huu huku kesi ya naibu rais mteule William Ruto ikianza mwezi wa tano.
No comments:
Post a Comment
TUPE MAWAZO YAKO