Polisi ya Saudi Arabia imewatia nguvuni raia 176 wakiwemo wanawake 15 kwa madai ya kukusanyika kinyume cha sheria wakitaka wanaharakati wa Kiislamu wanaoshikiliwa kwenye jela za nchi hiyo waachiliwe huru. Msemaji wa Polisi ya Saudia amesema watu hao walikamatwa jana baada ya kukataa kutawanyika mbele ya ofisi za Idara ya Upelelezi na Mashtaka huko Buraida katikati mwa nchi hiyo. Wanawake na watoto wao wamekuwa wakikusanyika katika vikundi vidogo vidogo huko Buraida kaskazini mwa mji mkuu wa Saudia Riyadh kutaka jamaa zao waliotiwa nguvuni waachiliwe huru. Shirika la kutetea haki za binadamu la Amnesty International limetoa taarifa ya kukosoa vikali utiaji mbaroni wa raia uliofanywa na polisi ya Saudia. Kwa mujibu wa Amnesty wanawake waliokusanyika hapo jana walikuwa wanadai kuachiwa huru jamaa zao wanaoshikiliwa pasina kufunguliwa mashtaka au kuhukumiwa, pamoja na wale wanaoendelea kusota gerezani licha ya kupita muda wa kutumikia vifungo vyao. Jumuiya za kutetea haki za binadamu nchini Saudia zimeripoti kuwa kuna wafungwa wa kisiasa wapatao elfu 30 katika jela za nchi hiyo ya Kifalme ambayo sheria zake zinapiga marufuku watu kuandamana
No comments:
Post a Comment
TUPE MAWAZO YAKO