Thursday, April 18, 2013

BAHRAIN YIAMARISHA USALAMA KABLA YA MASHINDANO YA FORMULA ONE


Katika kukaribia mashindano ya magari ya Formula One nchini Bahrain, hali ya usalama nchini humo imeimarishwa zaidi kuliko huko nyuma. Imepangwa kuwa, mashindano hayo ya mbio za magari yatafanyika nchini humo kwa muda wa siku tatu kuanzia Ijumaa Aprili 19 hadi Jumamosi Aprili 21. Tangu siku 5 zilizopita hadi sasa pia wananchi wa Bahrain wamekuwa wakiandamana kupinga kufanyika mashindano hayo ya magari ya Formular One na pia kuunga mkono harakati za mapinduzi ya nchi hiyo. Wabahrain wanaamini kuwa, utawala wa kifalme wa Aali Khalifa kwa kufanya mashindano hayo unataka kuonyesha kuwa hali ya nchi hiyo ni ya kawaida na kufunika matukio yanayojiri nchini. Hivi sasa mji mkuu wa Bahrain, Manama unazingirwa na vikosi vya usalama, vinavyotumia siasa za kuwakandamiza waandamanaji ili kufanya jitihada za kuandaa mazingira ya kufanyika kwa utulivu na maani mashindano hayo.  Lakini swali linaloulizwa hapa ni kuwa, je, ukandamizaji na kuzusha machafuko kunaweza kuficha na kufunika ukweli unaojiri katika jamii?
Kwa miaka miwili sasa Bahrain imekumbwa na mgogoro mkubwa uliosababisha mashindano hayo ya magari yasifanyike mwaka 2011. Lakini mwaka 2012 utawala wa Aali Khalifa ulifanya mashindano hayo kwa kustafidi na uungaji mkono wa vikosi vya usalama vya Saudia, huku mashindano hayo yakichanganyika na mambo mengine. Hii ni kwa sababu  wakati wa kufanyika mashindano hayo kulishtadi vurugu na kukandamizwa wananchi huku watu wengi wakiwa wahanga wa machafuko hayo. Lakini mwaka huu wananchi na wapinzani wa Bahrain wamesisitiza kuendelea na malalamiko yao dhidi ya hatua kama hizo za kimaonyesho, licha ya ukandamizaji wa utawala wa kifalme wa Aali Khalifa. Wamesema kuwa kuanzia siku ya Ijumaa yatakapoanza mashindano ya magari ya Formula One  nao pia wataanza maaandamano yaliyoratibiwa. Hii ni katika hali ambayo, viongozi wa Bahrain sambamba na kuwatishia wananchi kwamba watakabiliwa na adhabu kali, wanawafuatilia ili kuzusha woga na wasiwasi. Baadhi ya hatua zinazoshukuliwa na watawala wa Manama katika kukaribia mashindano hayo ni kushambulia mashule, kuzidi kuwatia mbaroni waandamanaji na kuwalenga wananchi wasio na ulinzi na risasi zilizojazwa hewa, hatua ambazo zinaharibu zaidi hali ya ndani ya nchi hiyo.  Nukta ya kuzingatiwa hapa ni kuwa, huku hali ikiwa hivyo watawala wa Bahrain wamependekeza kufanyika mazungumzo ya kitaifa. Tangu mwanzoni utawala wa Aali Khalifa ulipopendekeza suala hilo  wapinzani wa Bahrain walilitilia shaka jambo hilo na kusema kuwa, mazungumzo hayo  yanataka kutumiwa ili kupotosha fikra za waliowengi. Hivi sasa pia baada ya utawala huo wa kifalme kupoteza uhalali wa kisiasa wa kutawala, huku ukikabiliwa na malalamiko ya wananchi, unafanya jitihada ya kujipatia tena itibari na heshima katika uga wa kimataifa kwa kutumia mashindano hayo ya mbio za magari pamoja na mpango wa mazungumzo ya kitaifa. Wananchi wanamapinduzi wa Bahrain pia wamelifahamu hilo na sasa wamejipanga vilivyo ili kukabiliana na njama hizo za utawala wa Aali Khalifa. Wapinzani wa nchi hiyo wameitaka jamii ya kimataifa badala ya kushiriki kwenye mashindano hayo ya mbio za magari ilaani ukiukwaji haki za binadamu na ukandamizaji wa utawala wa Bahrain na kuunga mkono matakwa ya wananchi yanayodhihirishwa kwa maandamano ya amani kwa kususia mashindano hayo. 

No comments:

Post a Comment

TUPE MAWAZO YAKO