Kushtadi vitisho vya kila leo vya utawala wa Kizayuni wa Israel na kukithiri vitendo vyake vya kukiuka anga na mamlaka ya kujitawala Lebanon ni mambo ambayo yamepokewa kwa radiamali kali za Walebanon. Kuongezeka chokochoko za utawala wa Kizayuni wa Israel dhidi ya Lebanon kunabainisha nukta hii kwamba, njama za Wazayuni dhidi ya nchi hiyo ya Kiarabu hazina kikomo na kwamba, Tel Aviv inasubiri tu ipatikane fursa ili iivamie na kuikalia kwa mabavu nchi hiyo. Viongozi na shakshia mbalimbali wa Kilebanon wamelaani vikali hatua za kupenda kujitanua za Israel, huku Sheikh Nabir Qaouq, Naibu Mwenyekiti wa Baraza la Utendani la Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Hizbullah ya Lebanon akiionya Israel kwamba, isithubutu kuchukua hatua yoyote ile ya kiuadui dhidi ya Lebanon. Sheikh Nabir Qaouq ameashiria harakati za Israel za kutaka kufanya operesheni ya kiuadui dhidi ya Lebanon na kusema kuwa, vikosi vya muqawama viko macho na tayari tayari wakati wowote kwa ajili ya kukabiliana na adui Mzayuni. Naibu Mwenyekiti wa Baraza la Utendani la Hizbullah amezungumzia pia mgogoro wa Syria na kusema kuwa, kama nguvu na uwezo wa wanamuqawama wa Lebanon ungekuwa haujathibiti kivitendo kwa Israel, basi utawala huo ungekuwa umeshaishambulia kijeshi Lebanon ukitumia vibaya mgogoro wa Syria. Ameongeza kuwa, miongoni mwa mambo yanayopewa kipaumbele na muqawama wa Lebanon katika mipango yake ni kujiandaa kwa ajili ya kukabiliana na aina yoyote ile ya chokochoko za Israel na kwamba, Tel Aviv imekwishaonja mara kadhaa uchungu wa kipigo cha muqawama wa wananchi wa Lebanon. Msimamo imara wa Hizbullah unasisitizwa katika hali ambayo, Rais Michel Suleiman wa Lebanon amekosoa vikali hatua ya utawala wa Kizayuni wa Israel ya kuendelea kutoa vitisho dhidi ya nchi yake. Michel Suleiman ameashiria vitendo vya kichokozi vya mara kwa mara vya Israel vya kukiuka anga ya Lebanon na kubainisha kwamba, Wazayuni wangali wanaichokoza Lebanon. Ameitaka jamii ya kimataifa na Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa ambavyo vimekuwa vikionesha wasi wasi kuhusu utulivu na uthabiti wa Lebanon kuushinikiza utawala wa Kizayuni usitishe vitisho vyake dhidi ya Lebanon. Rais wa Lebanon amesisitiza kuwa, amani na utulivu wa Mashariki ya Kati utapatikana tu kwa kukomeshwa jinai na kusitishwa vitendo vya uchochezi vya utawala wa Kizayuni. Licha ya kuweko malalamiko makubwa ya walimwengu, lakini Israel inaendelea kukanyaga maazimizo ya Umoja wa Mataifa kutokana na kukiuka kwake mara kwa mara anga ya Lebanon. Kwa mujibu wa maazimio ya Umoja wa Mataifa kuhusiana na Lebanon hususan maazimio nambari 425 na 1701 ya Baraza la Usalama, Israel inapaswa kuheshimu haki ya kujitawala Lebanon na ardhi yote ya nchi hiyo. Hata hivyo Israel daima imekuwa ikipuuza maazimio hayo na badala yake kukiuka anga, ardhi na bahari ya Lebanon huku maeneo ya mashamba ya Shab'a na miinuko ya Kfar Shuba na Ghajar yakiwa yangali yanakaliwa kwa mabavu na utawala huo ghasibu.
No comments:
Post a Comment
TUPE MAWAZO YAKO