Siku moja baada ya Korea Kaskazini kuadhimisha mwaka wa 101 tangu kuzaliwa kwa mwasisi wa taifa hilo, nchi hiyo leo imeitaka Korea Kusini kuomba radhi kutokana na vitendo vyake vya kiadui na imetishia kuwa inaweza ikalipiza kisasi muda wowote. Taarifa hiyo ya jeshi la Korea Kaskazini, inaeleza kuwa Korea Kusini inapaswa kuomba radhi kutokana na waandamanaji mjini Seoul kuchoma sanamu za viongozi wa Korea Kaskazini. Korea Kaskazini imesema haitokubali mazungumzo yoyote na Korea Kusini, hadi nchi hiyo itakapoomba radhi kwa kitendo chake cha kihalifu. Hata hivyo, wizara ya ulinzi ya Korea Kusini, imesema haijapokea rasmi muda wa mwisho wa kuomba radhi, ikibainisha kuwa hakuna mawasiliano kati ya mataifa hayo mawili ya Korea. Wakati huo huo, jana Marekani imesema kuwa Rais Barack Obama na mwenzake wa Korea Kusini, Park Heun-Hye watakutana Mei 7 mwaka huu, katika Ikulu ya Marekani, kujadiliana kuhusu masuala ya kiuchumi na usalama.
No comments:
Post a Comment
TUPE MAWAZO YAKO