Rais wa Syria Bashar Al-Assad ametangaza msamaha wa jumla kwa uhalifu uliofanywa katika nchi hiyo inayokumbwa na vita. Chini ya amri hiyo ya rais, hukumu ya kifo sasa itabadilishwa na kuwa kifungo cha maisha gerezani na kazi ngumu. Tangazo hilo la sasa la msamaha halitawahusisha watu waliopatikana na hatia ya kufanya biashara haramu za silaha au uhalifu unaohusiana na dawa za kulevya, lakini wale walioshtakiwa na kuhukumiwa kwa kujiunga na uasi watapewa hukumu nyepesi. Hata hivyo wanaharakati nchini humo wamesema hatua hiyo haina maana yoyote kama hatawaachilia huru maelfu ya wafungwa wa kisiasa wanaoaminika kuwekwa kizuizini. Amri hiyo ya leo imetangazwa na kituo cha televisheni ya taifa SANA, lakini haikutangaza idadi ya wafungwa watakaopunguziwa hukumu. Amri kadhaa za msamaha zimetolewa tangu mgogoro huo ulipoanza nchini humo lakini hazijafanya lolote kuwaridhisha wanaharakati wa upinzani ambao wanasema wafungwa wengi wanazuiliwa na wengine hawajulikani waliko.
No comments:
Post a Comment
TUPE MAWAZO YAKO