“Harakati za Fatah na Hamas zimeshaipita awamu ya uhasama, na harakati ya Hamas inakubaliana na kuundwa serikali itakayoongozwa na Mahmoud Abbas”. Hayo ni matamshi yaliyotolewa na Musa Abu Marzouq, Naibu Mkuu wa Idara ya Kisiasa ya Harakati ya Muqawama wa Kiislamu ya Palestina HAMAS alipozungumza na waandishi wa habari juzi Jumanne kuelezea uwezekano wa kuundwa serikali mpya ya maridhiano ya kitaifa ya Palestina. Katika mazungumzo hayo na waandishi wa habari Abu Marzouq alitoa ufafanuzi wa vikao vya kutafuta mwafaka wa maridhiano ya kitaifa baina ya Wapalestina vilivyofanyika hivi karibuni mjini Cairo Misri, lengo hasa likiwa ni kuondoa mpasuko wa ndani baina ya harakati na taasisi za Kipalestina za Gaza na Ramallah na kueleza kwamba Hamas inakaribisha kuundwa kwa serikali ijayo itakayoongozwa na Mahmoud Abbas, Rais wa Mamlaka ya Ndani ya Palestina ambayo itaandaa mazingira ya kufanyika uchaguzi huko Palestina.
Musa Abu Marzouq alizungumzia pia mpango wa John Kerry, Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani wa ubadilishanaji ardhi kwa suluhu kati ya Wapalestina na utawala wa Kizayuni na kuundwa dola la Kiyahudi katika ardhi zinazokaliwa kwa mabavu za Palestina na kusisitiza kwamba lengo la mpango huo ni kuzihodhi kikamilifu ardhi zote za Palestina.
Kwa mtazamo wa viongozi wa Hamas ili kuweza kumaliza hitilafu za ndani, Mahmoud Abbas anapaswa kuyatambua rasmi makundi yote ya Palestina yanayotaka kushiriki kwenye uchaguzi wa Baitul Muqaddas na kuandaa mazingira ya kufanyika uchaguzi huru utakaoshirikisha makundi yote ya Palestina huko Ufukwe wa Magharibi wa Mto Jordan.
Safari ya hivi karibuni ya Mahmoud Abbas katika Ukanda wa Gaza iliyofanywa kwa lengo la kuleta umoja kati ya eneo hilo na lile la Ufukwe wa Magharibi ilipokewa kwa mikono miwili na viongozi wa Hamas; na hivi sasa Gaza inasubiri kwa hamu hatua muhimu inayopaswa kuchukuliwa na Rais wa Mamlaka ya Ndani ya Palestina ya kuunda serikali ya umoja wa kitaifa ili kufungua njia ya kufanyika chaguzi mbili muhimu za bunge la Palestina na Rais wa Mamlaka ya Ndani. Na hasa kwa kuzingatia kwamba hivi karibuni Mahmoud Abbas mwenyewe alitamka bayana kuwa siasa za utawala wa Kizayuni wa Israel ni za kutaka kujitanua na kwamba ujenzi wa vitongoji vya walowezi wa Kizayuni ndicho kizuizi kikuu cha kuanza kufanya tena mazungumzo na utawala huo ghasibu. Hii inamaanisha pia kwamba baada ya kupita miaka 20 ya mazungumzo na Israel viongozi wa Mamlaka ya Ndani ya Palestina wameshafika mwisho wa njia na wanahisi kuwa kuendelea na safari hiyo kutawaelekeza kusikojulikana. Mahmoud Abbas amesisitiza kwamba viongozi wa Palestina wanafungamana na suluhu kamili na ya kiadilifu itakayowahakikishia kuwa wanafikia lengo lao la kuunda nchi huru ya Palestina katika mipaka ya mwaka 1967. Kesho Ijumaa, Abbas anatazamiwa kukutana na kufanya mazungumzo na Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani John Kerry huko Ramallah. Itakumbukwa kuwa tangu tarehe 23 Machi mwaka huu Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani ameanzisha harakati za kuyafufua mazungumzo yaliyokufa kati ya Mamlaka ya Ndani ya Palestina na utawala wa Kizayuni wa Israel, hata hivyo harakati hizo za kidiplomasia za White House hadi sasa zimegonga ukuta kutokana na siasa za kushupalia vita na za kujitanua za utawala haramu wa Israel.
No comments:
Post a Comment
TUPE MAWAZO YAKO