Thursday, May 23, 2013

IRAN YALAANI MATAMSHI YA MAREKANI JUU YA UCHAGUZI


Iran imelaani vikali matamshi yasiyo na msingi ya serikali ya Marekani kuhusu mfumo wa uchaguzi nchini na kuingilia mambo yake ya ndani.
Katika taarifa, msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran Seyyed Abbas Araqchi amesema wakuu wa Marekani hawaufahamu mfumo wa uchaguzi wa Iran na wanakiuka sheria za kimsingi za kimataifa kwa kuingilia masuala ya ndani ya Iran. Amesema matamshi ya wakuu wa Marekani ni tusi kwa ufahamu na ustawi wa kisiasa wa watu wa Iran. Araqchi ameongeza kuwa taifa la Iran na waliowengi duniani wameshuhudia namna kwa zaidi ya nusu karne iliyopita Marekani ilivyokuwa ikiunga mkono tawala za kidikteta duniani kinyume na madai yake ya kuunga mkono demokrasia. Araqchi ametoa jibu hilo baada ya Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani Patrick Ventrell kukosoa Baraza la Kulinda Katiba la Iran kwa uamuzi wake wa kuwaondoa mamia ya watu waliokuwa wamejiandikisha kugombea katika uchaguzi wa rais nchini. Araqchi amesema wakuu wa Marekani wanapaswa kujifunza kuhusu mfumo wa uchaguzi wa Iran kabla ya kutoa matamshi yasiyo na msingi. Kati ya watu 686 waliojiandikisha kugombea urais ni wagombea wanane waliotimiza masharti na hivyo kuidhinishwa kugombea urais katika uchaguzi utakaofanyika Juni 14.

No comments:

Post a Comment

TUPE MAWAZO YAKO