Daniel Nevo Balozi wa utawala wa Kizayuni wa Israel mjini Amman Jordan, ameshinikizwa kuondoka nchini humo. Muhammad al Momani Waziri wa Habari na Mawasiliano wa Jordan amezungumza na vyombo vya habari na kuthibitisha tukio hilo. Nchi za Syria, Jordan, Misri na Lebanon zinapakana na utawala huo wa Kizayuni. Huku, Syria na Lebanon zikiwa hazina uhusiano rasmi na utawala huo ghasibu, Misri na Jordan zina mashirikiano rasmi na utawala huo baada ya kutiliana saini nao mikataba ya amani. Uhusiano rasmi kati ya Jordan na Israel ulianza baada ya kutiwa saini makubaliano ya amani yaliyojulikana kwa jina la "Wadi 'Araba" mwaka 1994. Tokea hapo uhusiano wa Amman na Tel Aviv uliendelea kuboreka hadi kufikia mwaka 2011.
Mara baada ya kuanza wimbi la mwamko wa Kiislamu wa wananchi katika eneo la Mashariki ya Kati na kaskazini mwa Afrika na kupelekea kuanguka tawala za madikteta wa Kiarabu, kama vile Zein al Abidine bin Ali wa Tunisia, Hosni Mubarak wa Misri na Muammar Gaddafi wa Libya, suala hilo pia liliwachochea wananchi wa Jordan na kusababisha uhusiano wa nchi hiyo na Israel kuingia dosari. Moja kati ya sababu kuu za kuibuka mwamko wa Kiislamu katika nchi hizo ni kukabiliana na harakati za Wazayuni, ambapo mara kadhaa wananchi wa nchi zilizo na uhusiano wa kidiplomasia na utawala wa Israel wamechoma moto bendera za utawala huo ghasibu wakitaka ukatwe uhusiano wa nchi zao na utawala huo bandia.
Nchini Jordan pia, kumeshuhudiwa harakati kadhaa za wananchi, vyama na makundi ya kisiasa yakionyesha hisia zao hizo dhidi ya Wazayuni. Wimbi la malalamiko ya wananchi wa Jordan katika kipindi cha miaka miwili ya hivi karibuni limeongezeka na hata kuulazimisha utawala huo kufunga virago nchini humo. Hasira na ghadhabu za wananchi wa Jordan zimeshadidi dhidi ya Israel, kutokana na nyendo na matamshi ya kijuba yanayotolewa mara kwa mara na viongozi wa utawala huo. Miongoni mwa mambo yanayowakasirisha Wajordan, ni sisitizo la Wazayuni la kutaka Wapalestina wote wahamishiwe nchini Jordan, na kuwa kama nchi yao mbadala. Njama hiyo ya Wazayuni ndiyo iliyoamsha hasira za Wajordan na hivyo kuharibu uhusiano wa pande mbili. Hivi karibuni mgogoro huo uliongezeka na kuingia katika hatua mpya baada ya balozi wa Israel mjini Amman kulazimishwa kuondoka nchini humo.
Hatua ya kuondoka balozi huyo huko Amman, imetokana pia na taathira za matukio yanayoendelea kujiri katika eneo. Mwendelezo wa vitendo vya walowezi wa Kizayuni wa kuuvunjia heshima Masjidul Aqswa na mashambulizi ya ndege za Israel katika ardhi ya Syria, ni miongoni mwa mambo yaliyowakera mno wabunge wa Jordan. Wiki iliyopita, wabunge hao walimtaka balozi wa Israel aondoke nchini Jordan kufuatia kushadidi malalamiko na maandamano ya wananchi wa nchi hiyo dhidi ya Israel. Hatua hiyo iliipelekea Wizara ya Mambo ya Nchi za Nje ya Jordan kumtimua balozi huyo nchini humo.
Nukta muhimu ni hii kwamba, uhusiano wa Jordan na Israel umeharibika katika hali ambayo wimbi jipya la mwamko wa Kiislamu katika Mashariki ya Kati na kaskazini mwa Afrika linaendelea kushika kasi. Utawala wa Israel umekuwa ukiitumia Jordan kama lango la kuingia bila matatizo katika nchi za Kiarabu. Hata hivyo kuzorota kwa uhusiano wa pande hizo mbili, licha ya kufunga lango hilo la kuelekea kwenye ulimwengu wa Kiarabu, kutaiweka pia Israel katika hali ngumu zaidi kwa kuzingatia matukio yanayojiri sasa katika eneo
No comments:
Post a Comment
TUPE MAWAZO YAKO