Tuesday, July 02, 2013

WAZIRI WA FEDHA URENO AJIUZULU

Waziri wa Fedha wa Ureno, Vitor Gaspar, amejiuzulu. Gaspar alikuwa ndiye mwenye dhamana ya kuhakikisha kuwa mageuzi muhimu yanafanyika kwenye mfumo wa kifedha na kiuchumi, chini ya mpango wa uokozi wa Umoja wa Ulaya na Shirika la Fedha la Kimataifa, IMF. Sasa, Mkuu wa Hazina, Maria Luis, ambaye amekuwa akisimamia juhudi za ubinafsishaji za nchi hiyo, ndiye atakayechukua nafasi ya Gaspar. Katika barua yake ya kujiuzulu, Gaspar amesema kwamba heshima yake kama waziri wa fedha ilikuwa ikihujumiwa kutokana na hatua za uokozi za Umoja wa Ulaya na IMF, ambazo zimeipa nchi hiyo euro bilioni 78. Wiki iliyopita, shirika la takwimu la nchi hiyo lilitangaza kwamba robo ya kwanza ya bajeti ya nchi hiyo ilikuwa na nakisi ya kiasi cha asilimia 10.6, wakati ambapo inatakiwa ipunguze nakisi hiyo hadi asilimia 5.5 ya pato lake la jumla mwaka huu. Ukosefu wa ajira unatazamiwa kupanda hadi asilimia 18.2, ambapo kwa vijana tayari umeshafikia asilimia 42. 

No comments:

Post a Comment

TUPE MAWAZO YAKO