Rais Uhuru Kenyatta wa Kenya amesema serikali yake haibabaishwi na mitazamo ya nchi za Magharibi ambazo zimekuwa zikimpiga vita. Akizungumza na wananchi katika barabara ya Nyeri-Nairobi, Rais Kenyatta amesema mitazamo ya nchi za Magharibi haitaizuia serikali ya Jubilee kuwahudumia Wakenya. Amesema lengo lake kuu ni kufanya kazi kwa bidii na kuinua uchumi wa Kenya. Rais Kenyatta amesema serikali yake itapata mafanikio makubwa na kwamba maadui wa Kenya watashangazwa na mafanikio yatakayopatikana nchini humo.
Matamshi ya Kenyatta yamekuja punde baada ya kubainika kuwa Rais Barack Obama wa Marekani atalitembelea bara la Afrika mwezi ujao lakini hatafika Kenya katika safari yake ya pili barani humo. Obama anatazamiwa kuzitembelea Senegal, Afrika Kusini na Tanzania. Obama sawa na marais waliomtangualia, Bill Clinton na George W Bush hataitembelea Kenya alikotoka baba yake mzazi. Kiongozi wa Waliowengi katika Bunge la Kenya Adan Duale amesema Nairobi haikumualika Obama na hivyo anaweza kuitembelea nchi yoyote aitakayo. Naye Mkuu wa Kamati ya Sera za Kigeni na Ulinzi katika Bunge Ndung’u Githinji amesema Kenya sasa hivi inazingatia ustawishaji uhusiano na nchi muhimu zinazoibuka duniani na kupuuzilia mbali hatua ya Obama ya kutotembelea Kenya akisisitiza kuwa uamuzi wa rais huyo wa Marekani hauna umuhimu kwa Kenya.
No comments:
Post a Comment
TUPE MAWAZO YAKO