Monday, May 13, 2013

MALI YATUMA ASKARI WAKE KARIBU MJI WA KIDAL

Serikali ya Mali imetangaza kuwa, imewapeleka askari wake karibu na mji wa Kidal kaskazini mashariki mwa nchi hiyo. Habari zaidi zinasema kuwa, hatua hiyo imefanyika kwa minajili ya kuusafisha mji huo kutokana na wanamgambo waasi. Kwa mujibu wa ripoti hiyo, serikali ya Mali inafanya juhudi za kuudhibiti mji huo, kabla ya uchaguzi wa bunge na rais uliopangwa kufanyika mwezi Julai mwaka huu. Siku ya Jumanne iliyopita, muungano wa viongozi wa jumuiya ya Waislamu nchini Mali, ulikosoa vikali hatua ya serikali kushindwa kutuma askari wake katika mji wa Kidal unaodhibitiwa na wanamgambo wa Kituareg. Hii ni katika hali ambayo, hivi karibuni kundi la Watuareg lilitangaza kuwa, litatoa jibu kali ikiwa askari wa Mali watajaribu kuingia katika ameneo yanayodhibitiwa na kundi hilo. Wakati huohuo Mawaziri wa ulinzi wa Jumuiya ya Kiuchumi ya Nchi za Magharibi mwa Afrika ECOWAS walikutana nchini Ivory Coast na kujadili hali ya mambo inayotawala nchini Mali, huku Waziri wa Mambo ya Nje wa Mali Tieman Kolibaly akimtaka Rais Blaisse Compaore wa Burkinafaso kufanya juhudi kubwa za kutuliza hali ya mambo katika mji wa Kidal ambao ungali unashikiliwa na waasi wa Tuareg.

No comments:

Post a Comment

TUPE MAWAZO YAKO