Friday, June 21, 2013

AL AZHAR WAPINGA FATWA YA MASHEIKH WA MISRI

Chuo Kikuu cha Kiislamu cha Al Azhar nchini Misri kimepinga vikali fatwa zilizotolewa na mashekhe wa Kiwahabi za kuwakufurisha wapinzani wanaoandamana kuipinga serikali ya Rais Mohammad Morsi wa nchi hiyo.
Katika taarifa, Al Azhar imesisitiza kuwa kupinga serikali kwa njia za amani ni jambo linaloruhusiwa na sheria za Kiislamu na kwamba hilo halina uhusiano wowote na imani au ukafiri.
Taarifa hiyo ya Al Azhar pia imetoa wito kwa Wamisri kuungana na kushikamana na kuonya kuhusu fitna mpya nchini humo. Al Azhar imesema fatwa za kuwakufurisha wapinzani zinatolewa na wanazuoni waliotoka katika mkondo sahihi wa Uislamu.
Katika siku za hivi karibuni kumeshuhudiwa ongezeko la maandamano dhidi ya utawala wa Rais Mohammad Morsi wa Misri.
Kiongozi mwandamizi wa upinzani Mohammad Al Baradei amesema kuwa, mapinduzi ya wananchi wa Misri yametokomezwa na kwamba Wamisri wanapaswa kumiminika tena mitaani tarehe 30 Juni kwa ajili ya kudumisha mapinduzi yao.

No comments:

Post a Comment

TUPE MAWAZO YAKO