Sunday, June 09, 2013

MAHAKAMA YEMEN YATAKA SALEH ACHUNGUZWE UPYA

Mahakama nchini Yemen imetoa amri ya kufanyika uchunguzi mpya kuhusu madai ya kuhusika dikteta wa zamani wa nchi hiyo Ali Abdullah Saleh katika mauaji ya waandamanaji 45 yaliyotokea mwaka 2011 wakati wa vuguvugu la maandamano dhidi ya utawala wake. Mahakama hiyo imeamuru maafisa 12 wa utawala wa Abdullah Saleh wahojiwe pia kuhusiana na tukio hilo lililotokea Machi 18 mwaka 2011 wakati askari na wafuasi wa dikteta huyo wa Yemen walipowafyatulia risasi raia waliokuwa wakiandamana dhidi ya utawala katika mji mkuu wa nchi hiyo Sanaa. Miongoni mwao ni Waziri wa zamani wa Mambo ya Ndani Jenerali Muther Al- Masri na mabinamu wawili wa Ali Abdullah Saleh ambao wote wawili walikuwa majenerali wa jeshi. Jaji Yahya Al- Ansi ameikataa rufaa ya upande wa mashtaka inayoeleza kwamba ombi la kutaka kumsaili Saleh ni batili kutokana na msamaha wa kutoshtakiwa aliopewa yeye na wasaidizi wake wa karibu kupitia mpango wa kukabidhi madaraka uliosimamiwa na Umoja wa Mataifa. Mnamo mwezi Februari Shirika la Kutetea Haki za Binaadamu la Human Rights Watch liliitaka Yemen ifanye uchunguzi huru kuhusu mauaji ya halaiki ya raia 45 wakati wa maandamano ya kupinga utawala wa kidikteta wa Ali Abdullah Saleh. Mamia ya watu waliuawa nchini Yemen wakati wa maandamano ya umma yaliyofanyika kwa muda wa mwaka mzima na kumlazimisha Saleh aondoke madarakani baada ya kuitawala Yemen kwa mkono wa chuma kwa muda wa miaka 33

No comments:

Post a Comment

TUPE MAWAZO YAKO