Friday, July 12, 2013

CIA WASEMA AL-QAEDA WAMETUMA ZANA ZA MABOMU LEBANON

Ikiwa ni siku kadhaa tangu kulipotokea shambulizi la kigaidi lililopelekea watu zaidi ya 50 kujeruhiwa na uharibifu mkubwa wa mali katika eneo la Bir al Abed la kusini mwa Beirut, mji mkuu wa Lebanon, Shirika la Kijasusi la Marekani CIA limeibuka na kutoa taarifa kwa vyombo vya usalama vya nchi hiyo kuwa, wanamgambo wa al Qaida wamepeleka mada za miripuko zenye uzito wa tani 16 kwa ajili ya kuyashambulia maeneo ya kusini mwa nchi hiyo. Katika ripoti yake ya kwanza CIA imesema kuwa, al Qaida wamekusudia kufanya mashambulizi mawili ya kujitolea muhanga dhidi ya makazi ya raia huko kusini mwa Lebanon. Amma katika ripoti yake ya pili CIA imesema kuwa, wanamgambo wa al Qaida, wameingiza nchini Lebanon mada za miripuko zenye uzito wa kilogramu 2000, kwa minajili ya kufanya mauaji dhidi ya jeshi, Hizbullah, balozi mbili za Saudia na Kuwait mjini Bairut na baadhi ya wanadiplomasia wa Russia na China walioko nchini humo. Hata hivyo weledi wa masuala ya kisiasa wameitaja hatua hiyo ya CIA kuwa ina lengo la kuivua Washingtona na shambulizi la hivi karibuni huko katika eneo la Bir al Abed la kusini mwa Beirut, kwa lengo la kulinda maslahi yake katika eneo hili hususan Lebanon, kutokana na kuhofia jibu linaloweza kutolewa na Harakati ya Hizbullah kama itashambuliwa.

No comments:

Post a Comment

TUPE MAWAZO YAKO