Friday, July 12, 2013

RAIS ASSAD ASEMA WAARAB WATAZINDUKA BAADA YA KUANGUKA MORSI

Rais Bashar al Assad wa Syria amesema kuwa, muundo wa Kiarabu unaanza kurejea kwenye njia yake sahihi, baada ya kuanguka Ikhwanul Muslimin na kufichuliwa uhakika wa mirengo ambayo inatumia dini kwa maslahi machache. Rais al Assad ameyasema hayo katika mahojiano na mwandishi wa habari wa gazeti la ‘Al-Baath’ na kuongeza kuwa, baadhi ya vyama ikiwemo Harakati ya Ikhwanul Muslimin vinatumia vibaya dini katika siasa. Aidha Rais wa Syria amewataka walimwengu kutofautisha baina ya wale wanaotumia dini kwa malengo yao binafsi, na wale wanaotumia dini katika kutetea kadhia muhimu za kisheria. Amewataja wanachama wa Ikhwan kuwa ni watu wenye misimamo mikali dhidi ya Waislamu wenzao na raia wenzao, huku wakijisahaulisha kabisa adui hatari yaani Israel na Magharibi. Wakati huo huo, magaidi walioko nchini Syia wamefanya mauaji ya umati dhidi ya watu 56 katika kijiji kimoja kaskazini mwa nchi hiyo. Habari zinasema kuwa, mauaji hayo yametokea mkoani Aleppo kaskazini mwa Syria na kwamba baada ya ukatili huo, magaidi hao wasio na ubinaadamu, wameitumbukiza miili ya marehemu hao katika shimo moja. Wengi wa wahanga wa mauaji hayo ni wanawake na watoto wadogo. Habari ya mauaji hayo, imefichuliwa baada ya askari wa Syria kulidhibiti eneo kulikojiri mauaji hayo.

No comments:

Post a Comment

TUPE MAWAZO YAKO