Tuesday, July 02, 2013

MACHAFUKO YAENDELEA LEBANON

Duru za habari nchini Lebanon, zinaelezea kuendelea kwa machafuko katika baadhi ya maeneo ya nchi hiyo. Kuhusiana na suala hilo, maadui na vibaraka wa nchi hiyo wamekuwa wakifanya harakati zenye lengo la kuzusha machafuko na fitina za kimadhehebu nchini humo. Wakati huo huo, mripuko uliosababishwa na bomu la kutupa kwa mkono lililotekelezwa na magaidi huko mjini Tripoli, kaskazini mwa nchi hiyo, limesababisha kwa uchache watu wawili kuuawa na wengine wanane kejeruhiwa. Katika siku za hivi karibuni, kumetokea mapigano kati ya waungaji mkono wa Rais Bashar al Assad wa Syria na wapinzani wake huko kaskazini mwa Lebanon na kupelekea watu kadhaa kati yao kuuawa na wengine kujeremiwa. Kwa sasa Lebanon inakabiliwa na mivutano ya kisiasa na machafuko, hali iliyowafanya Walebanon kuingiwa na wasiwasi wa kuhamia nchini mwao mgogoro wa Syria. Aidha Lebanon inakabiliwa na matatizo ya kiusalama katika miezi ya hivi karibuni, kutokana na kuongezeka kwa fitina na uchochezi wa Masalafi katika baadhi ya miji ya nchi hiyo, ukiwemo mkoa wa Tripoli kaskazini mwa nchi. Hii ni katika hali ambayo wanamgambo wanaopata himaya na uungaji mkono kutoka kwa kundi lenye kufuata siasa za Maghagibi la Machi 14 nchini humo, wamewashambulia wafuasi wa Kialawi mjini Tripoli eti kwa kumuunga mkono Rais Bashar al-Assada wa Syria. Kutokana na machafuko ya hivi karibuni mjini hapo, vikosi vya jeshi la Lebanon kwa kushirikiana na askari wa kulinda usalama nchini humo, wanapiga doria katika maeneo na barabara zote za mji huo, ili kurejesha hali ya usalama na amani nchini. Inasemekana kuwa, jeshi la Lebanon lilianza kuweka doria hiyo tangu mwezi Aprili mwaka 2013 kwa minajili ya kuimarisha usalama na amani mjini Tripoli na baadhi ya maeneo ya nchi hiyo. Alaakullihal, kushadidi kwa harakati za magaidi nchini Syria na kuongezeka uungaji mkono wa wafadhili wao huko Lebanon, kumewatia wasiwasi mkubwa viongozi wa serikali ya Beirut, kutokana na uwezekano wa kuhamia mgogoro huo nchini humo. Kuhusiana na suala hilo, Martin Nasirki Msemaji wa Umoja wa Mataifa ameashiria onyo lililotolewa hivi karibuni na Ban Ki-moon, Katibu Mkuu wa umoja huo kuhusu mgogoro wa Syria. Ni wazi kuwa mapigano na jinai zinazotekelezwa huko Syria mbele ya kimya cha jimii ya kimataifa, ni jambo lililopangwa kwa muda mrefu na magaidi hao pamoja na waungaji mkono wao wa kieneo na kimataifa. Duru za kisiasa nchini Lebanon zinaamini kuwa njama za kuzusha machafuko nchini humo, zilizoshadidi katika miezi ya hivi karibuni, ni kadhia nzito na hatari inayowalazimu wananchi kushirikiana kwa karibu na viongozi wao ili kuzivunja.

No comments:

Post a Comment

TUPE MAWAZO YAKO