Shirika la Afya duniani limearifu kuuawa watu 71 katika mapigano ya wanamgambo ndani ya mji wa bandari wa Kismayo kusini mwa Somalia. Ripoti ya (WHO) iliyotolewa leo imeeleza kuwa, mapigano hayo ya hivi karibuni yamesababisha pia idadi kubwa ya wakazi wa mji huo kuwa wakimbizi, watu 71 kuuawa na wengine zaidi ya 300 kujeruhiwa. Mji wa Kismayo, umegeuka na kuwa uwanja wa mapigano ya wanamgambo wanaotaka kuudhibiti tena baada ya kutwaliwa na serikali. Aidha mbali na wanamgambo, mji huo unakabiliwa na mapigano baina ya watu wa makabila kadhaa ambayo yanavutana kudai umiliki wa ardhi na kuingiza bidhaa zao katika mji huo wa pwani. Mwezi wa Oktoba mwaka jana, askari wa Kenya chini ya mwamvuli wa vikosi vya kulinda amani vya Umoja wa Afrika AMISOM, walifanikiwa kuudhibiti mji wa Kismayo, baada ya kuwafurusha wapiganaji wa As-Shabab mjini hapo. Bandari ya Kismayo iliyoko umbali wa kilometa 500 kutoka mji mkuu wa Mogadishu, ni eneo nyeti na ngome iliyosalia ya wanamgambo wa As-Shabab. Wakati huo huo Mjumbe maalumu wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa nchini Somalia, Bwana NicholasKay ameonyesha kusikitishwa kwake na machafuko katika mji huo na kuzitaka pande hasimu kufanya mazungumzo ya amani badala ya kutumia mtutu wa bunduki nchini humo.
No comments:
Post a Comment
TUPE MAWAZO YAKO