Marais wa mataifa ya Amerika ya kusini wanapanga mkutano wa dharura leo kujadili kuhusu kukatishwa kwa safari ya ndege iliyokuwa imemchukua rais wa Bolivia Evo Morales na kwenda Austria. Balozi wa Bolivia katika umoja wa mataifa amesema kuwa ndege ya Bolivia, ambayo ilikuwa imemchukua rais Morales wakati akirejea nyumbani kutoka mjini Moscow, ililazimishwa kutua na kukaguliwa mjini Vienna, Austria, kwa shaka ya kwamba mfanyakazi wa shirika la ujasusi la Marekani, Edward Snowden, huenda alikuwamo katika ndege hiyo. Uchunguzi uligundua kuwa Snowden hakuwamo katika ndege hiyo na iliruhusiwa kuendelea na safari mchana wa leo. Waziri wa mambo ya kigeni wa Bolivia David Choquehuanca amesema kuwa serikali yake inataka kujua nini kilichotokea.
Balozi wa Bolivia katika umoja wa mataifa, Sacha Llorenti, amewaambia waandishi habari mjini Geneva leo kuwa amefahamishwa kutakuwa na mkutano wa dharura wa viongozi wa umoja wa mataifa ya America ya kusini, UNASUR, lakini hakuna muda maalum uliopangwa kwa ajili ya mkutano huo. Rais Morales ameonesha kukasirishwa mno na hatua ya mataifa kadha ya Ulaya kutoiruhusu ndege yake kupita katika anga lao.
No comments:
Post a Comment
TUPE MAWAZO YAKO