Saturday, January 26, 2013

MAANDAMANO YA KUPINGA UTOAJI MIMBA YAFANYIKA MAREKANI


Maelfu ya wanaharakati wa haki za kuishi nchini Marekani jana Ijumaa wamekusanyika kwenye Mahakama Kuu nchini humo kupinga uamuzi wa kihistoria wa miaka 40 iliyopita wiki hii ambao umehalalisha utoaji mimba. Waandaaji wa matembezi ya mwaka kuhamasisha haki ya kuishi,huko Washington kwenye jengo la taifa la manunuzi,walitarajia umati mkubwa kupita ule uliojitokeza mwaka jana wa watu wapatao laki nne pamoja na uwepo wa baridi kali kwa sasa.
Kiongozi wa kanisa katoliki duniani Papa Benedicto wa 16 ameunga mkono maandamano hayo kwa kutuma ujumbe mfupi kupitia anwani yake ya mtandao wa twiter akiwatakia kila la heri wanaharakati hao na kusema kuwa anawaombea viongozi wa kisiasa ili walinde maisha ya watoto ambao bado hawajazaliwa na kuhamasisha utamaduni wa maisha.

VIKOSI VYA UFARANSA VYASONGA MBELE MALI

Vikosi vya Ufaransa na Mali vimesonga mbele kuelekea ngome muhimu ya waasi wenye itikadi kali za Kiislamu ya Gao, baada ya kuudhibiti tena mji wa kaskazini wa Hombori. Duru za vikosi vya usalama zimeeleza kuwa wanajeshi hao wataelekea Gao, moja ya miji mikubwa mitatu iliyopo eneo la kaskazini, ambako waasi wenye mafungamano na Al-Qaeda wameanzisha sheria ya Kiislamu ya Sharia kwa miezi kumi. Kwa mujibu wa duru hizo, katika eneo la magharibi mwa Mali, vikosi vinavyoongozwa na Ufaransa vinaelekea kwenye mji wa Lere kwa lengo la kuudhibiti mji wa Timbuktu uliopo kaskazini. Wakati huo huo, wakuu wa majeshi wa nchi za Afrika Magharibi wanakutana leo mjini Abidjan, Cote d'Ivoire katika kikao cha dharura kujadili operesheni za kijeshi nchini Mali zenye lengo la kuwaondoa waasi hao, ambapo watatathmini mchakato unaoendelea wa kupeleka vikosi vya kimataifa nchini Mali vinavyoongozwa na Afrika vya AFISMA. Aidha, viongozi wa Umoja wa Afrika wanatarajia kukutana Jumanne ijayo katika mkutano wa wafadhili ili kujadiliana kuhusu suala la kuongeza fedha katika operesheni za Mali. Mkutano huo utawajumuisha wawakilishi kutoka Umoja wa Ulaya na Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa.

WATANO WAUAWA MISRI KWENYE MAANDAMANO


Taarifa kutoka nchini Misri zinaeleza kuwa watu watano wameuawa na wengine kwa mamia wamejeruhiwa wakati wa maandamano ya kuadhimisha miaka miwili ya mapinduzi yaliyouondoa madarakani utawala wa Hosni Mubarak. Polisi walitumia mabomu ya kutoa machozi dhidi ya waandamanaji waliokuwa nje ya makaazi ya rais mjini Cairo. Ghasia zilizosababisha vifo na majeruhi hao zimetokea mjini Cairo na Alexandria pamoja na miji mingine ya Misri. Rais Mohammed Morsi ametoa wito wa kuwepo utulivu baada ya ghasia kati ya wapinzani na askari polisi.
Maandamano hayo yaliyoitishwa na viongozi wa upinzani yanaipinga serikali ya Rais Morsi aliyechaguliwa kwa kuzingatia demokrasia na anayeungwa mkono na vyama vya itikadi kali za Kiislamu. Upinzani unamshutumu Rais Morsi kwa kusaliti mapinduzi hayo.

MMAREKANI AHUKUMIWA MIAKA 494 JELA

Mahakama katika jimbo la Pennsylvania nchini Marekani imemuhukumu Walter Meyerle mwenye umri wa miaka 36 adhabu ya kifungo cha miaka 494 jela, baada ya kupatikana na kosa la kubaka na kuwadhalilisha kijinsia watoto 15 nchini humo. Mahakama hiyo imeeleza kuwa, kuanzia mwaka 1997 hadi 2010 Walter Meyerle aliwabaka watoto wavulana na wasichana wenye umri wa kati ya miaka  4 na 17. Mwendesha mashtaka wa kesi hiyo amesema kuwa, idadi kubwa ya watoto hao waliofanyiwa unyama huo walikuwa ni watoto wa marafiki zake. Wakati huohuo, Mahakama ya Chicago imempiga faini ya dola laki tano  mwalimu Kevin Jones baada ya kupatikana na hatia ya kuwadhalilisha wanafunzi wake. Mmoja kati ya mwanafunzi aliyekuwa mhanga wa kutumiwa vibaya kijinsia na mwalimu Kevin Jones alitoa ushadidi wake huo kwenye mahakama hiyo.

HATUA YA KOREA KASKAZINI KUJARIBU SILAHA ZAKE YATIA KIWEWE NCHI ZA MAGHARIBI

Hatua ya jana ya Korea Kaskazini ya kutangaza nia yake ya kufanyia majaribio ya nyuklia kama hatua ya kukabiliana na vitisho vya Marekani, imeutia kiwewe na woga mkubwa Umoja wa Ulaya na Marekani. Bi. Catherine Ashton, Mkuu wa Siasa za Mambo ya Nje wa Umoja wa Ulaya, ameitaka Korea Kaskazini kuachana na nia yake hiyo na kufuata mkondo wa kisiasa na kufanya mazungumzo na jamii za kimataifa. Jana ikulu ya Marekani pia ilitangaza kuwa, mpango wa Korea Kaskazini wa kufanya majaribio ya nyuklia, unatia wasiwasi mkubwa na kwamba, hatua hiyo itapelekea kutengwa kimataifa nchi hiyo. Msemaji wa Ikulu ya Marekani Jay Carney aliwaambia waandishi wa habari kuwa, hatua ya Pyongyang ya kutangaza nia yake kufanya majaribio ya nyuklia, inapingana na azimio la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa. Kwa upande wake Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya China Hung Lee, amezitaka nchi husika kukaa kwenye meza ya mazungumzo na Korea Kaskazini na kusisitiza kuwa, hiyo ndio njia pekee ya kumaliza mzozo uliopo. Hii ni katika hali ambayo, hivi karibuni Washington ilifanya jaribio la silaha za maangamizi ya umati chini ya ardhi huku jamii ya kimataifa ikiendelea kuwa bubu mbele ya hatua kama hizo za Marekani.

MAREKANI HAWAJAAFIKIANA KUHUSU SILAHA


Duru za habari kutoka Marekani zinaarifu kuwa, wapingaji na waungaji mkono wa uuzwaji silaha za moto nchini humo wameshindwa kuafikiana kuhusiana na kadhia ya kupiga marufuku uuzaji wa silaha hizo nchini humo. Duru za habari kutoka Congress ya Marekani zinasema kuwa bunge hilo Marekani linajadili muswada wa marufuku ya uuzwaji silaha unaofahamika kwa jina la Fainstein, ambao kama utapitishwa utapiga marufuku uuzwaji wa aina 160 ya silaha kwa raia nchini humo. Mkuu wa Kamisheni ya Wananchi mjini New York anayehusika na mpango wa kukabiliana na vitendo vya jinai Richard Aybom amesema kuwa, muswada wa huo wa Fainstein ni moja ya juhudi za Rais Barack Obama wa Marekani za kupunguza vitendo vya mauaji vilivyoshika kasi zaidi katika siku za hivi karibuni nchini humo. Wakati huo huo Eric Pratt Kiongozi Mkuu wa Mahusiano ya Umma katika Taasisi inayohusika na watu wanaomiliki silaha nchini Marekani amesema kuwa, kwa uzoefu wake muswada huo hauwezi kumaliza vitendo vya jinai na mauaji vinavyotokana na silaha zinazomilikiwa na raia nchini Marekani.

NAFASI YA WAISLAM NA KATIBA MPYA TANZANIA - USTADH ILUNGA


Friday, January 25, 2013

MAJESHI YA CHAD YAWASILI NIGER KUELEKEA MALI

Kundi kubwa la magari ya deraya na magari mengine yaliyobeba askari wa Chad kuelekea nchini Mali, limewasili mji mkuu wa Niamey nchini Niger. Vikosi hivyo vya Chad vinaelekea nchini Mali kwa ajili ya kushiriki katika oparesheni za kijeshi dhidi ya waasi wa nchi hiyo wanaoyadhibiti maeneo ya kaskazini. Kwa mujibu wa ripoti iliyotolewa na serikali ya Chad, vikosi hivyo vitaweka kambi katika mji wa Ouallam uliopo umbali wa kilometa 100 kaskazini mwa mji mkuu wa Niger, Niamey. Askari wa Niger wapatao 500 wapo katika eneo la mpakani. Hii ni katika hali ambayo, hadi sasa Chad ina wanajeshi wapatao 400 huko Niger. Hatimaye askari wa Chad na Niger wataelekea nchini Mali na kupiga kambi katika mji wa Gao kaskazini mwa nchi hiyo. Utumwaji wa askari hao unafanyika chini ya mwamvuli wa Jumuiya ya Kiuchumi ya Magharibi mwa Afrika (Ecowas) iliyopitisha azimio la kutumwa askari wa nchi wanachama wa jumuiya hiyo wapatao 3300 huko nchini Mali kwa ajili ya kuwatokomeza waasi wa kaskazini mwa nchi hiyo.

UFARANSA YAHARIBU VITUO VYA WAASI WA MALI

Ndege za kivita za Ufaransa zimeviharibu vituo viwili vya wapiganaji wa Kiislamu kaskazini mwa Mali, wakati ambapo kuna ripoti kuwa waasi hao wamegawanyika katika makundi mawili, moja likitaka kufanya mazungumzo ili kukomesha mashambulizi dhidi yao. Pia kumekuwepo na taarifa za majeshi ya Mali kufanya mauaji ya kinyama, ambapo kundi moja la haki za binaadamu limesema kuwa watu wasiyopungua 31 waliuawa katika mji wa kati wa Sevare, na maiti zao kutupwa katika visima. Chanzo kutoka duru za jeshi kimesema kuwa mashambulizi ya ndege yaliyofanyika usiku yamelenga vituo vilivyoko Ansongo, kilomita 80 kutoka mji wa Gao, na vituo vya kijeshi vya waasi vilivyoko katika kijiji jirani cha Seyna Sonrai. Jana Alhamisi, kundi jipya lililojitenga na Ansar Deen la Islamic Movement for Azawad, lilisema katika taarifa yake kuwa linapinga itikadi kali na ugaidi, na kwamba limedhamiria kupambana navyo, na kuongeza kuwa linataka suluhu ya muafaka ya mgogoro huo.

AHMED NEJAD ASISITIZA WAISLAM WOTE KUSHIKAMANA

Rais Mahmoud Ahmadinejad wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amewataka Waislamu kote duniani kuungana na kuzima njama za maadui. Rais Ahmadinejad ameyasema hayo leo, katika sherehe za kumalizika kwa mashindano ya Kimataifa ya Qur'ani Tukufu ya vikosi vya majeshi ya nchi za Kiislamu, yaliyofanyika mjini hapa Tehran kwa mnasaba wa kuwadia uzawa wa Mtukufu Mtume Muhammad (SAW) na wiki ya Umoja. Akizungumzia udharura wa kuimarishwa umoja kati ya Waislamu wote duniani Rais Mahmoud Ahmadinejad amesema kuwa, kuibua migongano na mizozo kati ya Waislamu ni mbinu zinazofanywa na maadui kwa ajili ya kuzusha mifarakano kati yao.
Amesema kuwa, maadui mara zote wamekuwa wakifanya njama za kuanzisha mivutano ya kikabila, kikaumu na kimadhehebu na kuongeza kuwa, pamoja na hayo Qur'ani na Mtume Muhammad ni thamani za Waislamu wote duniani bali pia ni kwa ajili ya watu wote wakiwemo wafuasi wa dini tofauti za mbinguni ikiwemo Uyahudi na Ukristo na walimwengu wote kwa ujumla. Kwa upande mwingine Rais Mahmoud Ahmadinejad amesema kuwa, moja ya sababu zinazopelekea kuzushwa mivutano, ni kutokufahamu tafsiri halisi ya Qur'ani na kwamba, suala hilo kwa muda mrefu limekuwa ndio chanzo cha matatizo kati ya Waislamu.

MATAIFA YA MAGHARIBI YATAKA RAIA WAKE KUONDOKA BENGHAZI

Uingereza, Ujerumani, Uholanzi na Australi zimewataka raia wake kuondoka katika mji wa Benghazi mashariki mwa Libya, kutokana na kitisho dhidi ya raia wa nchi za Magharibi, kinachohusishwa na kuingilia kijeshi kwa Ufaransa katika mgogoro wa Mali. Onyo la Uingereza lililotolewa jana Alhamisi liliikasirisha serikali ya Libya, iliyosema kuwa hakukuwa na taarifa mpya za uchunguzi kuhalalisha wasi wasi huo mjini Benghazi. Idara ya mambo ya nje ya Australia imesema kuwa wanatambua tishio maalumu kwa raia wa nchi za Magharibi mjini Benghazi, na kuwataka raia wake kuondoka huko mara moja. Waziri Mkuu wa Uingereza David Cameron alionya wiki iliyopita kuwa kilichotoekea nchini Algeria katika kiwanda cha gesi ni sehemu tu ya vita virefu dhidi ya magaidi wauaji duniani kote. Jana Alhamisi, Ujerumani na Uholanzi pia ziliwaonya raia wake na kuwataka waondoke mara moja kutoka Benghazi. Lakini naibu waziri wa mambo ya kigeni wa Libya, Abdullah Massoud alielezwa kusikitisha kwake juu ya onyo hizo, na kusema kuwa serikali mjini Tripoli itahitaji maelezo.

MISRI YAUPINGA MKATABA WA AMANI WA CAMP DAVID

Duru za kidiplomasia kutoka Cairo zinaeleza kuwa, serikali ya Misri imetupilia mbali takwa la Marekani la kuitaka serikali hiyo ifungamane kikamilifu na makubaliano ya amani ya Camp David yaliyotiwa saini kati ya Misri na utawala wa Kizayuni wa Israel. Hatua ya serikali ya Misri ya kukataa pendekezo hilo, hivi karibuni ilipelekea hata Washington kutuma ujumbe maalumu ulioongozwa na Seneta John Mc Cain kuwashawishi viongozi wa Cairo kufungamana na makubaliano ya Camp David. Baadhi ya viongozi wa Misri wamesikika wakisema kuwa, siyo jambo la kimantiki kwa Cairo kufungamana na makubaliano hayo.
Makubaliano ya amani ya Camp David yalitiwa saini kati ya Anwar Sadat Rais wa zamani wa Misri na Menachem Begin Waziri Mkuu wa zamani wa utawala wa Kizayuni wa Israel tarehe 17 Septemba 1978, chini ya usimamizi wa Jimmy Carter Rais wa zamani wa Marekani.

UN YARIDHIA DRONE KUTUMWA KONGO

Baraza la Umoja wa Mataifa limeidhinisha matumizi ya ndege zisizo na rubani, mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo, baada wiki kadhaa za ucheleweshwaji kufuatia wasi wasi wa Urusi, China na Rwanda juu ya matumizi ya ndege hizo za uchunguzi. Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa ban Ki-Moon aliliandikia Baraza hilo mwishoni mwa mwezi uliyopita, kushauri kuwa walinda amani nchini Kongo wanapanga kutumia ndege hizo kuboresha uwelewa wa hali ya huko na kuharakisha mchakato wa maamuzi katika kushughulikia uasi wa kundi la M23. Rais wa baraza hilo kwa mwezi huu wa Januari, balozi wa Pakistan katika Umoja wa Mataifa Masood Khan amemjibu Katibu Mkuu Ban kuwa wamepokea maombi hayo na kuyaridhia. Lakini baraza hilo limesema ndege hizuo zitatumika tu kwa majaribio.
 

KOREA KASKAZINI YATISHIA KUISHAMBULIA KUSINI

Korea Kaskazini imetishia kuishambulia Korea Kusini, kama utawala mjini Seoul utaunga mkono vikwazo vipya vya Umoja wa Mataifa dhidi ya nchi hiyo. Onyo hilo la Korea Kaskazini limetolewa wakati ambapo Marekani imetangaza vikwazo zaidi vya kiuchumi dhidi ya Korea Kaskazini, kufuatia hatua ya nchi hiyo kutuma roketi ya setilaiti angani mwezi uliyopita. Korea Kaskazini imemuonya jirani wa kusini kuwa vikwazo vinamanisha kutangaza vita dhidi yao. Korea Kaskazini ilitangaza wiki hii kususia mazungumzo yote yanayolenga kusitisha mpango wake wa nyuklia, na kuapa kufanya majaribio zaidi ya roketi na nyuklia, baada ya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kuituhumu kwa jaribio la kombora la masafa marefu Desemba mwaka jana.

WAZAYUNI WAMECHOCHEA MARUFUKU YA KANALI ZA IRAN

Wabunge kadhaa nchini Uhispania wameikosoa vikali serikali ya nchi hiyo kwa kupiga marufuku matangazo ya kanali za Televisheni za Press TV na Hispan TV kutokana na mashinikizo ya lobi za Kizayuni na Marekani. Katika barua yao, wabunge wa chama cha United Left wameitaka serikali ya Uhispania kutoa maelezo iwapo Waziri wa Mambo ya Nje wa Uhispania Jose Manuel Garcia-Margallo alijadili suala la kupiga marufuku kanali za Iran wakati alipokutana na lobi za Kizayuni Oktoba mwaka 2012. Wabunge hao wamesema mmiliki wa shirika la satalaiti ya Eutelsat ana uraia wa Israel na kwamba amekuwa akiongoza njama dhidi ya vyombo vya habari vya Iran barani Ulaya.
Televisheni ya Iran ya Hispan TV hurusha matangazo kwa lugha ya Kihispania kwa masaa 24 nayo Press TV hurusha matangazo yake kwa lugha ya Kiingereza. Hivi karibuni televisheni za kimataifa za Iran Hispan TV pamoja na Press TV zilipigwa marufuku kurusha matangazo yao kupitia satalaiti za Ulaya za Eutelsat na Hotbird. Aidha Shirika la Intelsat limepiga marufuku matangazo ya radio na televisheni kadhaa za kimataifa za Iran kufuatia mashinikizo ya Umoja wa Ulaya. Maamuzi hayo ya kupiga marufu vyombo vya habari vya Iran ni ishara ya wazi ya undumakuwili wa nchi za Magharibi zinazodai kutetea uhuru wa maoni. Nchi za Ulaya na Marekani zikishirikiana na utawala wa Kizayuni wa Israel zinajaribu kuzima sauti ya haki ya vyombo vya habari vya Iran.