Tuesday, March 26, 2013

FAMILIA YA GADDAFI YAPEWA HIFADHI OMAN


Waziri wa Mambo ya Nchi za Nje wa Libya Muhammad Abdulaziz amesema kuwa, baadhi ya watu wa familia ya aliyekuwa kiongozi wa nchi hiyo Muammar Gaddafi wameondoka nchini Algeria na wamepewa hifadhi nchini Oman.
Matamshi ya Abdulaziz yanatolewa katika hali ambayo, siku chache zilizopita vyombo vya habari vya Oman vilitangaza kuwa, baadhi ya watu wa familia ya Gaddafi wamepewa hifadhi nchini humo kwa sababu za kibinadamu akiwemo aliyekuwa mke wa Gaddafi. Taarifa zinasema kuwa, watu waliopewa hifadhi ni wanawake na watoto wenye umri wa chini ya miaka 18 na hawataruhusiwa kujishughulisha na shughuli za kisiasa au kuzungumza na vyombo vya habari.
Inafaa kuashiria hapa kuwa, baada ya mji mkuu wa Libya, Tripoli kuanguka mikononi mwa wafanyamapinduzi, Safiya mke wa Gaddafi pamoja na binti yake Ayesha, na watoto wa kiume Hannibal na Muhammad walikimbilia nchini Algeria mwezi Agosti 2011.
Watoto wengine wa kiume wa Gaddafi, Saad yuko mafichoni nchini  Niger, Mu'utassim na Khamis waliuawa kwenye mapigano,  Seiful A'rab aliuawa kwenye mashambulio ya anga ya majeshi ya Nato na Seiful Islam alitiwa mbaroni nchini Libya mwezi Novemba 2011.

CHOMSKY ASEMA MWISHO WA ISRAEL UNAKARIBIA


Mwandishi mashuhuri wa Marekani Noam Chomsky amesema kuwa, utawala wa Kizayuni wa Israel hatimaye utatokomea kutokana na kuwa na mtenguko wa kimaadili na kutengwa kimataifa.
Akihojiwa na gazeti la Guardian la Uingereza, Chomsky amesema kuwa, siasa za kutaka kujitanua za utawala wa Israel zimepelekea kuporomoka kimaadili na kutengwa utawala huo. Amesisitiza kuwa, hatima ya utawala huo ghasibu ni kutokomea na tukio hilo haliko mbali.
Akizungumzia mahusiano ya nchi za Magharibi na wanamapinduzi katika nchi za Kiarabu, mwanafikra huyo wa Kimarekani amesema kuwa, uchunguzi wa maoni unaonyesha kuwa, wananchi walio wengi nchini Misri yaani baina ya asilimia 80 hadi 90 wanaziangalia tawala za Marekani na utawala wa Israel kuwa ni tishio lao kuu.

GEREZA LA BAGRAM LAKABIDHIWA KWA WAAFGHANISTAN


Marekani imeikabidhi Afghanistan udhibiti kamili wa gereza la Bagram, hatua ambayo imeondoa kizingiti kikubwa katika uhusiano baina ya nchi hizo mbili, wakati majeshi ya kimataifa yanayoongozwa na Marekani yakijiandaa kuondoka nchini Afghanistan, baada ya vita vya zaidi ya muongo mmoja.
Kamanda wa vikosi vya kimataifa nchini Afghanistan, Jenerali Joseph Dunford, amesema katika taarifa yake kwamba makabidhiano hayo yanaonyesha kuimarika na kujiamini kwa Afghanistan. Bagram lilikuwa gereza pekee chini ya udhibiti wa Marekani nchini Afghanistan, na serikali za nchi mbili zilikubaliana mwaka mmoja uliopita kuwa lingekabidhiwa kwa Afghanistan.
Rais  Hamid Karzai wa Afghanistan alikuwa amekuita kukabidhiwa gereza hilo kama hatua muhimu ya kurejesha uhuru wa nchi yake juu ya masuala muhimu kutoka kwa Marekani. Marekani kwa upande wake ilikuwa na wasiwasi kwamba kulikabidhi gereza hilo lenye wafungwa wa Taliban na al-Qaida kwa serikali dhaifu ya Afghanistan, kungewapa fursa wafungwa hao kurudi kwenye uwanja wa vita. 

ULAYA NA JAPAN ZAKUBALIANA KUANZA MAZUNGUMZO


Japan na Umoja wa Ulaya wamekubaliana kuanzisha mazungumzo kuelekea mojawapo ya mikataba muhimu kabisa ya biashara ulimwenguni. Hatua hiyo imefikiwa licha ya upinzani kutoka makampuni ya kutengeneza magari barani Ulaya.
 Waziri Mkuu wa Japan, Shinzo Abe, Rais wa Halmashauri ya Ulaya, Jose Manuel Barroso, na Rais wa Baraza la Ulaya, Herman van Rompuy, wamefanya mazungumzo ya simu juu ya mpango huo, baada ya viongozi wa Ulaya kuahirisha safari ya kwenda Tokyo kutokana na mgogoro wa kifedha wa Cyprus.
Japan na Ulaya wanaazimia kuimarisha ushirikiano ambao utajumuisha theluthi moja ya uchumi wa dunia, ambao unatatizwa na taratibu za kibiashara zinazizuia nchi nyingine kwenye soko lao. Muafaka katika mazungumzo hayo hautegemewei kupatikana kirahisi.

RAIS WA ZAMBIA AACHIWA KWA DHAMANA



Rais wa zamani wa Zambia, Rupia Banda ameachiliwa huru kwa dhamana baada ya kukamatwa na kupandishwa kizimbani kwa tuhuma za ufisadi na utumizi mbaya wa madaraka. Wakili wa Banda, Sakwiba Sikota amesema mteja wake hana hatia na kwamba ana imani mahakama itadhihirisha hilo. Sikota ameongeza kuwa, Banda ataanza kuhudhuria vikao vya mahakama hapo Kesho. Rupia Banda anatuhumiwa kuiba zaidi ya dola milioni 11 kutoka hazina ya taifa katika kipindi cha uongozi wake. Bunge la Zambia mapema mwezi huu lilimuondolea kinga ya kutoshtakiwa na hivyo kutoa fursa kwa polisi kumkamata na kumfungulia mashtaka. Banda amewaambia wafuasi wake nje ya korti kwamba yeye ni raia mwema anayefuata sheria za nchi na amewataka kuwa watulivu huku kesi yake ikiendelea. Banda aliingia madarakani Agosti mwaka 2008 baada ya kufariki dunia, Levy Mwanawasa na kisha kushinda kwenye uchaguzi wa rais miezi miwili baadaye. Alishindwa kutetea wadhifa wake kwenye uchaguzi wa mwaka 2011 aliposhindwa na mpinzani wake wa muda mrefu, Michael Sata.

MAHAKAMA YA JUU YA KENYA YATAKA KURA KUHESABIWA TENA BAADHI YA VITUO



Mahakama ya Juu nchini Kenya imeamuru kura zihesabiwe upya katika vituo 22, kufuatia uchaguzi wa urais ambao uliepuka duru ya pili kwa kura chache. Amri iliyotolewa na jaji wa mahakama hiyo hivi leo, Smokin Wanjila, imetaka kuhesabiwa upya kwa kura katika vituo hivyo, ambavyo ni kama chembe tu ya vituo 32,000 vilivyokuwepo katika uchaguzi wa Machi 4, kuanze kesho.
Pia nayo Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) imetakiwa kuweka wazi daftari la wapiga kura ililotumia kuhesabu kura, baada ya mfumo wa elektroniki kukwama. Matokeo rasmi ya uchaguzi huo yalimpa ushindi Uhuru Kenyatta, ambaye alivuuka mstari wa asilimia 50 kwa kura 8,000 tu.
Hata hivyo, Kenyatta alimzidi mpinzani wake wa karibu, Raila Odinga, kwa kura 800,000. Muungano wa CORD, unaoongozwa na Odinga, na mashirika kadhaa ya kiraia wamewasilisha kesi katika mahakama ya juu ya Kenya, wakilalamikia kile walichokiita hitilafu kubwa wakati wa uchaguzi.

MAREKANI INA MPANGO WA KUISHAMBULIA KIJESHI ISRAEL


Gazeti la Washington Post limeripoti kuwa jeshi la Marekani limeandaa mipango kadhaa ya kuishambulia kijeshi Syria ikiwemo kufanya mashambulio ya anga hadi kutuma vikosi vya wanajeshi ndani ya ardhi ya nchi hiyo kwa madai ya kile kilichodaiwa kuwa ni kudhibiti maeneo ya silaha za kemikali. Hata hivyo hadi sasa Washington inashindwa kufanya hivyo kwa kuchelea upinzani wa kisiasa dhidi ya uvamizi wake wa kijeshi na vilevile kukoesekana uratibu kati yake na nchi waitifaki katika eneo. “Kama tungepaswa kufanya hivyo kesho ningesema kwamba hatuko tayari” amesema afisa mmoja wa serikali ya Marekani ambaye hakutaka kutaja jina lake na kuongeza kuwa kitu kimoja wanachojaribu kuepuka ni kuwa na kundi moja la kulinda maeneo ya silaha za kemikali huku kundi jengine likishambulio maeneo hayo kwa makombora. Kufuatia ripoti za shambulio la silaha za kemikali lililofanywa karibu na mji wa Aleppo na makundi ya kigaidi nchini Syria yanayofadhiliwa kijeshi na kifedha na nchi za kigeni zikiwemo za Magharibi na za Kiarabu katika eneo, Rais Barack Obama wa Marekani alisema kuwa ameziagiza timu maalumu kufanya uchunguzi makini ili kujua kama mstari huo mwekundu umekiukwa au la. Ripoti zaidi zinaeleza kuwa serikali ya Obama inajaribu kutumia kila njia ili kuibebesha serikali ya Syria lawama za shambulio hilo la silaha za kemikali lililosababisha vifo vya raia kadhaa

WAZIRI MKUU WA UTURUKI AKATAA OMBI LA MSAMAHA LA ISRAEL

Recep Tayyip Erdogan Waziri Mkuu wa Uturuki amesema kuwa hatua ya Israel ya kuomba radhi pekee haitoshi kuhuisha uhusiano wa Ankara na Tel Aviv na kuongeza kuwa Tel Aviv inapasa kuahidi kabla ya pande mbili hizo kuhuisha uhusiano baina yao. Benjamin Netanyahu Ijumaa iliyopita alimpigia simu Waziri Mkuu wa Uturuki na  kumuomba radhi kufuatia kuuawa raia kadhaa wa nchi hiyo katika shambulizi lililofanywa na wanajeshi wa utawala wa Kizayuni  katika meli ya uhuru ya Flotilla huko Ghaza mwaka 2010. Hata hivyo Waziri Mkuu wa Uturuki alitangaza jana kuwa hakutakuwa na uhuishaji wa haraka wa uhusiano kati ya Ankara na Tel Aviv. Recep Tayyep Erdogan amesema hivi na hapa ninamnukuu, "tumeshasema uhusiano kati ya Israel na Uturuki hautahuishwa iwapo utawala wa Kizayuni hautaomba msamaha, hautalipa fidia na kuondoa mzingiro kwa Wapalestina", mwisho wa kumnukuu.

Monday, March 25, 2013

KERRY AINYA IRAQ JUU YA ANGA YAKE KUTUMIWA NA IRAN

Waziri wa Mambo ya nchi za Kigeni wa Marekani John Kerry ameishinikiza Iraq kuacha kuziruhusu ndege za Iran zinazodaiwa kusafirisha vifaa vya kijeshi kupitia anga zake kuelekea Syria. Akizungumza wakati wa ziara yake ya ghafla mjini Baghdad, Kerry amemwonya Waziri Mkuu wa iraq, Nuri al-Maliki kwamba Marekani inaangalia kile Iraq inachokifanya, hizo zikiwa ni shutuma kali kuwahi kutolewa dhidi ya serikali ya Iraq kwa kukosa kukagua safari za ndege ambazo Iran inasisitiza kuwa ni za kusafirisha misaada ya kibinaadamu pekee. Ziara hiyo ya siku moja, ambayo ni ya kwanza kufanywa na waziri wa mambo ya kigeni wa Marekani tangu mwaka wa 2009, pia imeangazia hofu ya Marekani kwamba vurugu za miezi kadhaa katika mikoa ya nchi hiyo inayokaliwa na Wasunni walio wengi zinaweza kuyapa nafasi ya kuendesha harakati zao makundi ya wanamgambo ikiwa ni pamoja na al-Qaeda.

MKUU WA WAPINZANI WA SYRIA AJIUZULU

Mkuu wa muungano wa wapinzani wa Syria amejiuzulu wadhifa wake huo. Ahmad Moaz al Khatib leo ametangaza kujiuzulu wadhifa wake huo kupitia ukursasa wake wa facebook. Kujiuzulu ghafla kwa Moaz al Khatib kumejiri baada ya muungano wa wapinzani wa Syria kumchagua Ghassan Hito kuwa Waziri Mkuu wa ile inayodaiwa kuwa serikali ya mpito ya makundi ya upinzani ya Syria. Awali kiongozi huyo wa muungano wa wapinzani wa Syria alisema kuwa ana mpango wa kujiuzulu kufuatia kushadidi hitilafu za ndani kati ya makundi yanayoipinga serikali ya Rais Bashar al Assad wa Syria. Katika upande mwingine wanajeshi wa Israel wamelirushia maroketi jeshi la Syria kutoka katika miinuko ya Golan inayokaliwa kwa mabavu na utawala wa Kizayuni wa Israel. Jeshi la utawala wa Kizayuni limesema kuwa wanajeshi wake walirusha maroketi hayo leo katika miinuko ya Golan. Moshe Yaalon, Waziri mpya wa masuala ya kijeshi wa Israel amesema kuwa, Tel Aviv itaendelea kuyakalia maeneo hayo. Milima ya Golan ni mali ya Syria lakini inakaliwa kwa mabavu na Israel huku makundi yanayojifanya kutetea haki za mataifa mengine yakiendelea kunyamazia kimya ubeberu huo. Huku hayo yakiripotiwa kundi kuu la wanamgambo wanaoendesha vitendo vya kigaidi nchini Syria linalojiita jeshi huru la Syria limekataa kumtambua Ghassan Hitto kuwa Waziri Mkuu wa eti serikali ya mpito ya wapinzani.

IKHWANUL MUSLIMINA WAITAKA UFARANSA KUONDOA VIKOSI VYAKE NCHINI MALI

Chama cha Ikhwanul Muslimin cha Misri kimesema kuwa, ukoloni wa Ufaransa nchini Mali hautadumu, na kimemtaka mkoloni huyo mkongwe wa Ulaya kuondoa vikosi vyake katika nchi hiyo ya magharibi mwa Afrika.
Rashad al Bayoumi, Naibu wa Mkuu wa kundi la Ikhwanul Muslimin la nchini Misri amesema hayo na kuongeza kuwa, wanataraji kuiona Ufaransa ikiangalia upya mahesabu yake vinginevyo itapata hasara kubwa huko Mali.
Vile vile ameufananisha uvamizi wa Ufaransa nchini Mali na uvamizi wa Marekani katika nchi za Afghanistan na Iraq.
Januari 11 mwaka huu, Ufaransa ilianzisha vita nchini Mali kwa madai ya kupambana na makundi ya kigaidi yaliyokuwa yameteka maeneo ya kaskazini mwa nchi hiyo.
Lakini Ufaransa hiyo hiyo ndiyo iliyoko mstari wa mbele katika kampeni za kuyapelekea silaha makundi hayo hayo nchini Syria licha ya kuwa imetuma vikosi vyake kuyapiga vita nchini Mali. Nchi za Magharibi za Marekani, Canada, Ubelgiji, Ujerumani na Denmark zimetangaza kuunga mkono uvamizi huo wa Ufaransa nchini Mali.
Uvamizi huo umesababisha matatizo mengi ya kibinaadamu nchini Mali huku maelfu ya watu wakipoteza makazi yao na wanaishi kwa kutangatanga.

Sunday, March 24, 2013

KUSHINDWA KWA VITA YA GHAZA ILIKUWA AIBU KWA ISRAEL

Mjumbe wa Kamisheni ya Usalama wa Taifa na Siasa za Nje ya  Bunge la Iran amesema kuwa, kushindwa utawala wa Kizayuni katika vita vya siku nane ulivyovianzisha mwaka jana huko Ghaza Palestina, kumewasha moto katika hema la kitambaa laini la utawala wa Kizayuni na matokeo yake yatakuwa ni kufutika kikamilifu utawala huo pandikizi katika uso wa dunia.
Bw. Muhammad Ridha Muhsini Thani amewaambia waandishi wa habari kuwa, muqawama na mapambano ya kishujaa ya wanamapambano wa Palestina katika vita hivyo vya siku nane yamethibitisha kuwa sasa wanamapambano hao hawatumii tena mawe na marungu kupambana na Wazayuni bali wamejizatiti kwa silaha za kisasa kukabiliana na jinai za Israel.
Mbunge huyo wa Iran pia amesema, kushindwa mfumo wa kujikinga na makombora wa utawala wa Kizayuni kuzuia makombora ya wanamapambano wa Palestina licha ya mfumo huo kuwa wa gharama kubwa, ilikuwa ni fedheha nyingine kubwa ya kisiasa na kijeshi iliyoikumba Israel na madola yanayoisaidia.
Itakumbukwa kuwa, mwaka jana utawala wa Kizayuni ulianzisha vita vingine dhidi ya Ukanda wa Ghaza na kujigamba kuwa vita hivyo vitachukua muda mrefu lakini wenyewe uliomba kusitisha vita hivyo katika siku ya nane tu baada ya makombora ya Wapalestina kupiga miji mikubwa kama vile Tel Aviv, mji mkuu wa utawala wa Kizayuni.

UN YAITAKA ISRAEL KUONDOA VITONGOJI VYAKE ARDHI YA WAPALESTINA


Baraza la Haki za Binadamu la Umoja wa Mataifa limeutaka utawala wa Kizayuni wa Israel uviondoe vitongoji vyote ulivyojenga katika Ufukwe wa Magharibi wa Mto Jordan wa ardhi za Palestina unazozikalia kwa mabavu. Kikao cha baraza hilo kilichofanyika siku ya Ijumaa, aidha kimeutaka utawala haramu wa Kizayuni ulipe fidia kwa hasara ulizowasababishia Wapalestina kutokana na ujenzi wa vitongoji hivyo. Kati ya nchi zote 47 wanachama wa Baraza la Haki za Binadamu la Umoja wa Mataifa ni Marekani pekee ndiyo iliyopinga uamuzi huo uliopitishwa na baraza hilo juu ya ulazima wa kuondolewa vitongoji vya walowezi wa Kizayuni katika ardhi za Palestina.
Marekani imeweka pingamizi ya kuzuia kulaaniwa utawala wa Kizayuni katika Baraza la Haki za Binadamu la Umoja wa Mataifa katika hali ambayo katika safari yake huko Palestina inayokaliwa kwa mabavu, Rais wa Marekani Barack Obama alijidai kutoa matamshi ya kimaonyesho ya kukosoa ujenzi wa vitongoji katika ardhi za Wapalestina. Migongano ya maneno na vitendo katika misimamo ya Marekani inadhihirisha jinsi nchi hiyo inavyozidi kutumia mbinu za hila na hadaa ili kuficha ukweli kwamba inaunga mkono kikamilifu siasa za kujipanua za utawala haramu wa Kizayuni. Inafaa kuashiria hapa kwamba wakati wa safari ya hivi majuzi ya Obama huko Palestina inayokaliwa kwa mabavu viongozi wa utawala wa Kizayuni walitangaza kuwa awamu mpya ya ujenzi wa vitongoji itaanza hivi karibuni. Yair Lapid, waziri mpya wa fedha wa utawala haramu wa Israel alitangaza siku ya Ijumaa kwamba utawala huo umeshapasisha mpango mpya wa kujenga maelfu ya nyumba katika maeneo ya Ufukwe wa Magharibi na Baitul Muqaddas. Lengo la utawala wa Kizayuni la kupanua vitongoji vya walowezi wa Kizayuni katika Ufukwe wa Magharibi unaoukalia kwa mabavu ni kulidhibiti kikamilifu eneo hilo na kuliunganisha na ardhi za Palestina zilizovamiwa na kuanza kukaliwa kwa mabavu mwaka 1948 na kupewa jina la Israel. Alaa kulli hal, kushadidi siasa za kujipanua za utawala wa Kizayuni katika maeneo ya Paletsina na hatua za Marekani za kupinga na kuzuia kulaaniwa kwa namna yoyote ile utawala huo ghasibu katika taasisi za kimataifa ni ithbati tosha kuwa Washington inatoa baraka kamili kwa Israel za kuendeleza siasa zake hizo katika Palestina unayoikalia kwa mabavu. Masuala hayo yanadhihirisha matokeo hasi ya safari ya Obama katika Mashariki ya Kati na vilevile kubainisha ukweli kwamba harakati mpya za Marekani katika eneo hili zinazotekelezwa katika kalibu ya kufufua mchakato wa mazungumzo ya mapatano kati ya Mamlaka ya Ndani ya Palestina na utawala wa Kizayuni wa Israel hazina lengo jengine ghairi ya kuzidi kuzipigisha mnada haki za Wapalestina, kuuzatiti na kuupa nguvu zaidi uvamizi na ukaliaji wa mabavu wa utawala wa Kizayuni na kuhalalisha sera za utawala huo ghasibu za kuzidi kujipanua katika ardhi za Palestina…

IRAN YAPINGA MADAI YA SAUDI ARABIA


Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran Ramin Mehmanparasat amepinga madai ya Saudi Arabia kuhusu kuwepo raia wa Iran katika mtandao wa majasusi waliokamatwa hivi karibuni nchini humo.
Ramin Mehmanparast  amekosoa vikali madai hayo ya maafisa wa Saudi Arabia na kusema madai hayo yamekuwa yakikaririwa mara kwa mara na hayana msingi wowote. Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran amesema madai hayo yasiyo na msingi yamesambazwa katika vyombo vya habari vya Saudia kwa lengo la kupotosha fikra za umma nchini humo.

ISRAEL NA SYRIA WAANZA KUSHAMBULIANA MILIMA YA GHOLAN

Jeshi la Israel limesema leo kuwa wanajeshi wake wamejibu mashambulizi yaliyofanywa kutoka upande wa Syria katika milima ya Gholan. Msemaji wa jeshi la Israel amesema milio ya risasi kutoka upande wa mpaka wa Syria ilifyatuliwa kuelekezwa upande wa kituo cha doria cha Israel. Hakuna ripoti za vifo au hasara iliyosababishwa kwa upande wa Israel. Haijabainika haraka kama milio hiyo ya risasi imefyatuliwa na wanajeshi wa Syria au waasi.