Friday, February 10, 2012

NINI TUNAJIFUNZA KAMA WAISLAM TUNAOTAKA MABADILIKO.


Baraza la Mitihani la Taifa (Necta) limetangaza matokeo ya Mitihani ya Kidato cha Nne (CSEE) iliyofanyika nchini Oktoba, mwaka jana, huku kiwango cha kufaulu kikionyesha kuwa kiasi cha asilimia 46.63 na cha kufeli kwa kupata daraja sifuri ni asilimia 53.37

Matokeo hayo yaliyotangazwa jana na Katibu Mtendaji wa Necta, Dk. Joyce Ndalichako, yanaonyesha kuwa, licha ya kiwango cha kufaulu kuongezeka kwa asilimia 3.13, bado wanafunzi wengi wameendelea kufanya bibaya katika mtihani huo.

Kwa mujibu wa matokeo hayo, kati ya watahiniwa 426,314 sawa na asilimia 94.67 waliofaulu kati ya daraja la kwanza hadi la nne ni 180,216.

Hata hivyo, waliofaulu kwa daraja la nne ndio wengi wakiwa ni 146,639 sawa na asilimia 81.3 ya waliofaulu huku wale wa daraja la kwanza, pili na tatu wakiwa ni 33,577 sawa na asilimia 9.8.

Wakati hali kwa watahiniwa ikiwa hivyo, shule za sekondari za kata, zimeendelea kufanya vibaya kulinganisha na zile za watu binafsi.

Pia watahiniwa 3,303 wamefutiwa matokeo kutokana na baadhi kufanya udanganyifu na wengine kuandika matusi katika karatasi zao za majibu ya mitihani.

Hata hivyo, matokeo hayo yanaonyesha wavulana wakiongoza kufaulu mitihani hiyo kwa asilimia 53.53, huku wasichana wakifaulu kwa asilimia 44.36.

WATAHINIWA WA SHULE WALIOFAULU MTIHANI

“Mwaka 2010 watahiniwa waliofaulu walikuwa 177,021 sawa na asilimia 50.40 ya watahiniwa waliofanya mtihani huo. Hivyo, kiwango cha kufaulu kimeongezeka kwa asilimia 3.13,” alisema Dk. Ndalichako. Ongezoko hilo ni sawa na watahiniwa 12,789.

WATAHINIWA WOTE

Alisema jumla ya watahiniwa 225,126 (asilimia 53.37) wamefaulu mtihani huo, wakiwamo wasichana 90,885 sawa na asilimia 48.25 ya wasichana waliofanya mtihani na wavulana 134,241 sawa na asilimia 57.51 ya wavulana waliofanya mtihani.

“Mwaka 2010 watahiniwa waliofaulu walikuwa 223,085 sawa na asilimia 50.74. hivyo, kufaulu kumeongezeka kwa asilimia 3.13,” alisema Dk. Ndalichako.

WALIOSAJILIWA KUFANYA MTIHANI

Alisema jumla ya watahiniwa 450,324 walisajiliwa kufanya mitihani hiyo, kati yao wakiwamo wasichana 201,799 (aslimia 44.81) na wavulana 248,525 (asilimia 55.19), idadi ambayo imepungua kwa watahiniwa 7,790 (asilimia 1.70) kati ya watahiniwa 458,114 waliosajiliwa mwaka juzi.

WALIOFANYA NA AMBAO HAWAKUFANYA MTIHANI

Dk. Ndalichako alisema watahiniwa waliofanya mtihani huo ni 426,314 (asilimia 94.67) na kwamba, watahiniwa 24,010 hawakufanya mtihani, ambao ni sawa na asilimia 5.33 ya watahiniwa wote waliosajiliwa.



WATAHINIWA WA SHULE WALIOSAJILIWA

Alisema watahiniwa wa shule waliosajiliwa ni 349,390 wakiwamo wasichana 150,371 (asilimia 43.04) na wavulana 199,019 (asilimia (56.96), idadi ambayo inaonyesha kupungua kwa watahiniwa 14,209 (asilimia 3.91) kati ya watahiniwa 363,589 wa shule waliosajiliwa mwaka juzi.

VITUO VYA MITIHANI

Dk. Ndalichako alisema jumla ya vituo 4,795 vilitumika katika kufanya mitihani hiyo ikilinganishwa na vituo 4,653 vilivyotumika mwaka juzi.

WALIOFAULU MTIHANI WA MAARIFA

Alisema katika Mtihani wa Maarifa (QT) wa mwaka jana, jumla ya watahiniwa 9,069 (asilimia 40.70) ya waliofanya mtihani wamefaulu ikilinganishwa na asilimia 35.17 ya waliofaulu mtihani mwaka juzi.

“Hivyo, kiwango cha kufaulu kwa Mtihani wa Maarufu kimeongezeka kwa asilimia 5.53 ikilinganishwa na mwaka 2010,” alisema Dk. Ndalichako.

Alisema katika mtihani huo, watahiniwa waliosajiliwa ni 29,447 ambapo wasichana walikuwa ni 18,019 na wavulana ni 11,428 na kwamba, jumla ya watahiniwa 22,400 (asilimia 76.07) ya waliosajiliwa wamefanya mtihani, wasichana wakiwa ni 13,898 na wavulana ni 8,502.

WATAHINIWA WA KUJITEGEMEA

Dk. Ndalichako alisema watahiniwa wa kujitegemea waliofaulu mtihani ni 44,910 (asilimia 52.52) ya waliofanya mtihani; wasichana wakiwa ni 20,972 (asilimia 47.90) na wavulana ni 23.938 (asilimia 57.38).

Alisema mwaka juzi watahiniwa wa kujitegemea walikuwa 46,064 (asilimia 52.09) walifaulu mtihani huo.

UBORA WA KUFAULU KWA JINSIA

Dk. Ndalichako alisema jumla ya watahiniwa wa shule 33,577 (asilimia 9.98) wamefaulu katika madaraja I-III; wasichana wakiwa 10,313 (asilimia 7.13 na wavulana 23,264 (asilimia 12.13).

SHULE BORA

Alizitaja shule 10 bora zilizoko katika kundi la shule zenye watahiniwa 40 na zaidi kuwa ni St. Francis Girls iliyoko mkoani Mbeya; Feza Boys (Dar es Salaam); St. Joseph Millenium (Dar es Salaam); Marian Girls (Pwani); Don Bosco Seminary (Iringa); Kasita Seminary (Morogoro); St. Mary’s Mazinde Juu (Tanga); Canossa (Dar es Salaam); Mzumbe (Morogoro) na Kibaha (Pwani).

Pia alizitaja shule 10 bora zilizoko katika kundi la shule zenye watahiniwa chini ya 40 kuwa ni Thomas More Machrina (Dar es Salaam); Feza Girls (Dar es Salaam); Dung’unyi Seminary (Singida); Maua Seminary (Kilimanjaro); Rubya Seminary (Kagera); St. Joseph Kilocha Seminary (Iringa); Sengerema Seminary (Mwanza); Lumumba (Unguja); Queen of Apostels-Ushirombo (Shinyanga) na Bihawana Junior Seminary (Dodoma).

SHULE ZA MWISHO

Vilevile, alizitaja shule 10 za mwisho zenye watahiniwa 40 na zaidi kuwa ni Bwembwera (Tanga); Pande Darajani (Tanga); Mfundia (Tanga); Zirai (Tanga); Kasokola (Rukwa); Tongoni (Tanga); Mofu (Morogoro); Mziha (Morogoro); Maneromango (Pwani) na Kibuta (Pwani).

Kadhalika, alizitaja shule 10 za mwisho zenye watahiniwa chini ya 40 kuwa ni Ndongosi (Ruvuma); St. Luke (Ruvuma); Igigwa (Tabora); Kining’inila (Tabora); Ndaoya (Tanga); Kilangali (Morogoro); Kikulyungu (Lindi); Usunga (Tabora); Mto Bubu Day (Dodoma) na Miguruwe (Lindi).

WANAFUNZI WALIOFANYA VIZURI ZAIDI

Aliwataja watahiniwa 10 bora kitaifa kuwa na shule wanazotoka kwenye mabano kuwa ni Moses Andrew Swai (Feza Boy’s-Dar es Salaam); Rosalyn Tandau (Marian Girls-Pwani); Mboni Maumba (St. Francis Girls-Mbeya); Sepiso Mwamelo (St. Francis Girls-Mbeya); Uwella Rubuga (Marian Girls-Pwani); Hellen Mpanduji (St. Mary’s Mazinde Juu-Tanga); Daniel Wallace Maugo (St. Joseph Millenium-Dar es Salaam); Benjamin Tilubuzya (Thomas More Machrina-Dar es Salaam); Simon William Mbangalukela (St. Joseph Millenium-Dar es Salaam) na Nimrod Deocles Rutatora (Feza Boy’s-Dar es Salaam).

WASICHANA 10 BORA KITAIFA

Pia aliwataja wasichana 10 bora kitaifa kuwa ni Rosalyn Tandau (Marian Girls-Pwani); Mboni Maumba (St. Francis Girls-Mbeya); Sepiso Mwamelo (St. Francis Girls-Mbeya); Uwella Rubuga (Marian Girls-Pwani); Hellen Mpanduji (St. Mary’s Mazinde Juu-Tanga); Lissa Chile (St. Francis Girls-Mbeya); Elizabeth Ng’imba (St. Francis Girls-Mbeya); Doris Atieno Noah (Kandoto Sayansi Girls-Kilimanjaro); Herieth Machunda (St. Francis Girls-Mbeya) na Daisy Mugenyi (Kifungilo Girls-Tanga).

WAVULANA 10 BORA KITAIFA

Vilevile, aliwataja wavulana 10 bora kitaifa kuwa ni Moses Andrew Swai (Feza Boy’s-Dar es Salaam); Daniel Wallace Maugo (St. Joseph Millenium-Dar es Salaam); Benjamin Tilubuzya (Thomas More Machrina-Dar es Salaam); Simon William Mbangalukela (St. Joseph Millenium-Dar es Salaam); Nimrod Deocles Rutatora (Feza Boy’s-Dar es Salaam); Simon Gabriel Mnyele (Feza Boys-Dar es Salaam); Paschal John Madukwa (Nyegezi Seminary-Mwanza); Henry Justo Stanley (St. Joseph Millenium-Dar es Salaam); Frasisco Paschal Kibasa (Mzumbe-Morogoro) na Tumaini Charles (Ilboru-Arusha).

MATOKEO YA MTIHANI YALIYOSITISHWA

Katibu Mtendaji huyo alisema Baraza limesitisha kutoa matokeo ya watahiniwa 264 wa kujitegemea waliofanya mtihani wa kidato cha nne, 116 waliofanya mtihani wa maarifa na 873 wa shule za binafsi mwaka jana bila kulipa ada ya mtihani hadi watakapolipa ada pamoja na faini.

Alisema ikiwa watahiniwa hao hawatalipa baada ya miaka miwili tangu matokeo yatakapotangazwa, matokeo yatafutwa.

Dk. Ndalichako alisema wengine ni watahiniwa 67 ambao hawajawasilishiwa alama za tathmini ya masomo (Continuous Assessment) katika masomo yote waliyofanya hadi hapo Mkuu wa Shule husika atakapowasilisha pamoja na sababu za kutowasilisha mapema.

WALIOFANYA UDANGANYIFU KATIKA MITIHANI

Alisema Baraza pia limefuta matokeo ya watahiniwa 3,303 waliobainika kufanya udanganyifu katika mitihani ya Oktoba mwaka jana; ambao kati yao alisema watahiniwa 3,301 ni wa mtihani wa kidato cha nne na wawili ni wa maarifa.

Alizitaja aina za udanganyifu zilizobainika kufanywa na watahiniwa hao kuwa ni pamoja na watahiniwa kukamatwa na wasimamizi ndani ya chumba cha mtihani wakiwa na notes, simu kufanyiwa mitihani na watu wengine na kubainika wamesajiliwa kufanya mtihani kwa kutumia majina ya wengine wakati walishafanya mtihani.

Aina nyingine za udanganyifu ni watahiniwa kubainika kuwa na mfanano wa majibu usio wa kawaida, kuwa na karatasi zao kuwa na miandiko tofauti au kuwa na miandiko tofauti katika katarasi ya somo moja, kubadilishana karatasi za maswali/vijitabu vya kujibia mtihani ili kuandikiana majibu, au kujadiliana ndani ya chumba cha mtihani.

Pia watahiniwa kukamatwa na vijitabu vya kuandika mitihani zaidi ya moja ambayo moja hakupewa na msimamizi, kubainika kuwa na kesi mbili tofauti; kama vile, mfanano wa majibu, notes, kijitabu cha kujibia zaidi ya kimoja na kubadilishana karatasi ya majibu au kijitabu cha kujibia mtihani.

WATAHINIWA WALIOANDIKA MATUSI

Dk. Ndalichako alisema matokeo mengine yaliyofutwa na Baraza ni ya watahiniwa wanane walioandika matusi katika karatasi za majibu yao.

Alisema kitendo hicho ni kosa kwa mujibu wa kifungu 5 (13) cha kanuni za mtihani.

Dk. Ndalichako alisema kitendo cha kuandika matusi kwenye karatasi za majibu, kinaonyesha utovu wa nidhamu wa hali ya juu na kwamba Baraza halitavumilia hata kidogo watahiniwa wa aina hiyo.

“Hivyo, pamoja na kuwafutia matokeo ufuatiliaji zaidi utafanyika ili kuona hatua zaidi wanazoweza kuchukuliwa,” alisema Dk. Ndalichako.

Aliwataka watahiniwa walioanza mitihani ya kidato cha sita jana kujiepusha na udanganyifu katika mitihani na pia kuepuka mtindo wa kuandika matusi katika skripti zao au mambo yasiyohusiana na mtihani.

HATMA YA WATAHINIWA WALIOFUTIWA MATOKEO

Alisema Baraza limekuwa likifuta matokeo ya watahiniwa wanaofanya udanganyifu, lakini idadi ya wanaojihusisha na vitendo hivyo imekuwa ikiongezeka mwaka hadi mwaka.

“Hivyo, katika kikao chake cha 86 kilichofanyika tarehe 7/2/2012, Baraza liliamua kuwa watahiniwa wote waliofutiwa matokeo yao kutokana na kujihusisha na udanganyifu au kuandika matusi kwenye karatasi zao za majibu hawataruhusiwa kufanya mtihani wa Baraza kwa kipindi kisichopungua miaka mitatu,” alisema Dk. Ndalichako.

VITUO NA WALIOHUSIKA NA UDANGANYIFU

Alitoa onyo kali kwa wamiliki wote wa vituo na shule ambazo zimejihusisha na udanganyifu.

“Tunapenda kuwajulisha wamiliki wote wa vituo vya watahiniwa wa kujitegemea kuwa ni wajibu ao kuhakikisha kuwa kanuni zote za uendeshaji mitihani zinazingatiwa ipasavyo,” alisema Dk. Ndalichako.

CHANZO: NIPASHE


No comments:

Post a Comment

TUPE MAWAZO YAKO