Wednesday, November 28, 2012

HIZBULLAH YAFANYA MAZOEZI YA KIJESHI NA KUIONYA ISRAEL PIA

Gazeti la Al Jamhuriyyah la Lebanon limeandika kuwa, hivi karibuni Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Hizbullah ya Lebanon ilifanya manuva kubwa ya kijeshi iliyowashirikisha wapiganaji shupavu wa harakati hiyo wapatao elfu 10.

Gazeti hilo limeendelea kuandika kuwa, manuva hiyo imefanyika kwa minajili ya kujiweka tayari kwa chokochoko zozote za utawala wa Kizayuni wa Israel na yalifanyika katika maeneo kadhaa ya kusini na mashariki mwa Lebanon. 

Aidha gazeti hilo limeandika kuwa, manuva hayo yalifanyika kwa muda wa siku tatu. Manuva hayo yaliyowashirikisha vijana wenye umri wa miaka 16 hadi 20 yanahesabiwa kuwa ya kwanza na ya aina yake ambayo yamewahi kufanywa na Hizbullah katika maeneo yaliyochini ya udhibiti wake.


Pia katibu Mkuu wa Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Lebanon Hizbullah ameuonya utawala wa Kizayuni wa Israel kwamba utakabiliwa na tsunami ya makombora yenye nguvu zaidi kuliko Fajr 5 katika miji yote ya Palestina inayokaliwa kwa mabavu ukiwemo Tel Aviv, iwapo utawala huo khabithi utaanzisha tena chokochoko dhidi ya ardhi ya Lebanon. Akizungumza na waumini waliokuwa wakiomboleza Ashura ya Imam Hussein AS kusini mwa Beirut, Sayyid Hassan Nasrullah amehoji kuwa, utawala wa Israel umetiwa kiwewe na makombora machache tu ya Fajr 5 yaliyorushwa na wapiganaji wa Hamas wa Kipalestina, vipi utaweza kustahamili kishindo cha maelfu ya makombora yenye nguvu zaidi ya Hizbullah yatakayokita kwenye miji yote ya utawala huo? Katibu Mkuu wa Hizbullah ameongeza kuwa, utawala wa Israel unaelekea kusambaratika kwani kwa muda mrefu umekuwa ukiingiwa na kitete mbele ya wanamuqawama.

No comments:

Post a Comment

TUPE MAWAZO YAKO