Friday, January 25, 2013

MAJESHI YA CHAD YAWASILI NIGER KUELEKEA MALI

Kundi kubwa la magari ya deraya na magari mengine yaliyobeba askari wa Chad kuelekea nchini Mali, limewasili mji mkuu wa Niamey nchini Niger. Vikosi hivyo vya Chad vinaelekea nchini Mali kwa ajili ya kushiriki katika oparesheni za kijeshi dhidi ya waasi wa nchi hiyo wanaoyadhibiti maeneo ya kaskazini. Kwa mujibu wa ripoti iliyotolewa na serikali ya Chad, vikosi hivyo vitaweka kambi katika mji wa Ouallam uliopo umbali wa kilometa 100 kaskazini mwa mji mkuu wa Niger, Niamey. Askari wa Niger wapatao 500 wapo katika eneo la mpakani. Hii ni katika hali ambayo, hadi sasa Chad ina wanajeshi wapatao 400 huko Niger. Hatimaye askari wa Chad na Niger wataelekea nchini Mali na kupiga kambi katika mji wa Gao kaskazini mwa nchi hiyo. Utumwaji wa askari hao unafanyika chini ya mwamvuli wa Jumuiya ya Kiuchumi ya Magharibi mwa Afrika (Ecowas) iliyopitisha azimio la kutumwa askari wa nchi wanachama wa jumuiya hiyo wapatao 3300 huko nchini Mali kwa ajili ya kuwatokomeza waasi wa kaskazini mwa nchi hiyo.

No comments:

Post a Comment

TUPE MAWAZO YAKO