Sunday, January 27, 2013

WATU KADHAA WAUAWA MISRI BAADA YA MAANDAMANO YA KUPINGA HUKUMU YA KIFO KWA WENZAO

Wizara ya Afya ya nchini Misri imetangaza kuwa, watu 40 wameuawa na wengine 277 wamejeruhiwa kufuatia ghasia zilizoibuka jana nchini humo. Machafuko hayo yalijiri baada ya Mahakama ya Jinai ya nchi hiyo kutoa hukumu ya kifo kwa watu 21 waliopatikana na hatia ya kushiriki katika ghasia za Februari mwaka jana mjini Port Said katika uwanja wa soka baada ya mechi iliyozikutanisha klabu mbili za al Ahly na al Masry. Jeshi la Misri limeimarisha doria Port Said ili kurejesha hali ya amani na usalama. Waandamanaji waliokuwa na hasira kali walishambulia na kuteketeza moto ofisi kadhaa mjini hapo ikiwemo jela na jengo la shirika la umeme. Ghasia hizo zilizuka baada ya kundi moja la waandamanaji kuvamia gereza linalosadikiwa kuwa na watuhumiwa hao na kuanza kuwafyatulia risasi askari wa usalama. Wizara ya Mambo ya Ndani ya Misri imetangaza kuwa, askari kadhaa wameuawa na wengine 150 wamejeruhiwa katika tukio hilo. Ghasia hizo zimempelekea Rais Muhammad Mursi wa nchi hiyo kufuta safari yake mjini Addis Ababa Ethiopia kwa ajili ya kushiriki mkutano wa wakuu wa Umoja wa Afrika.

No comments:

Post a Comment

TUPE MAWAZO YAKO