Saturday, February 02, 2013

AI YALAANI UKIUKAJI HAKI ZA KIBINADAMU NCHINI MALI


Shirika la Msamaha Duniani la Amnesty International limelaani ukiukaji mkubwa wa haki za binadamu yakiwemo mauaji ya watoto wadogo katika vita vya Ufaransa huko nchini Mali.
Taarifa ya Amnesty International imebainisha kwamba, ushahidi unaonesha kuwa, kuna kesi nyingi za ukiukaji wa haki za binadamu nchini Mali tangu Ufaransa ilipoanza kufanya mashambulio yake ya kijeshi kaskazini mwa nchi hiyo Januari 11 mwaka huu. Raia wa Mali wamekuwa wakiuawa kufuatia mashambulio ya anga ya Ufaransa na kesi ya karibuni kabisa ni kuuawa watoto watatu wa nchi hiyo.
Ripoti ya Amnesty International imetolewa baada ya kufanyika uchunguzi wa siku kumi huko Mali kuhusiana na hali ya haki za binadamu katika nchi hiyo ya magharibi mwa Afrika. Taarifa hiyo imeongeza kuwa, uingiliaji wa kijeshi wa Ufaransa nchini Mali ulifanyika kwa kisingizio cha kukomesha mapigano katika nchi hiyo lakini kivitendo hali ya machafuko nchini humo imeshadidi.
Shirika la Msamaha Duniani la Amnesty International limelaani pia vitendo vya kuwanyonga raia vinavyofanywa na jeshi la Mali na kusisitiza kwamba, vitendo hivyo ni ukiukaji mkubwa wa haki za binadamu na ukanyagaji wa sheria za kimataifa.

No comments:

Post a Comment

TUPE MAWAZO YAKO