Thursday, February 28, 2013

NJAMA ZA MAREKANI KUVIBAKIZA VIKOSI VYA UFARANSA NCHINI MALI

Uingiliaji kijeshi wa Ufaransa nchini Mali umepelekea serikali ya Paris kukabiliwa na matatizo mbalimbali kama vile ya kifedha, kilojistiki na pia kudhamini askari jeshi kwa ajili ya kikosi maalumu cha kutoa mafunzo kwa wanajeshi wa Mali. Viongozi wa Ufaransa wanasema kuwa, uingiliaji huo umewagharimu mamilioni ya yuro. Licha ya yote hayo kupelekea viongozi wa Paris waanze kuratibu mipango ya kuondoa askari wao nchini Mali lakini Marekani inapinga suala hilo. Kwa kuzingatia kwamba imepangwa kuwa askari wa Ufaransa waanze kuondoka nchini Mali mwezi Machi, maseneta kadhaa wa Marekani waliotembelea Mali hivi karibuni, kwa kutoa kisingizo kuwa bado hali ya uthabiti ya nchi hiyo haijaimarika wamesisitiza kuendelea kuwepo askari wa Ufaransa nchini humo. Hii ni katika hali ambayo, kurejea nyuma wapinzani wa serikali ya mpito ya Mali na kutimuliwa katika miji ya kaskazini mwa nchi hiyo kumeandaa mazingira ya kuondoka taratibu wanajeshi wa Ufaransa nchini humo kuanzia mwezi Machi mwaka huu.  
Kwa msingi huo, kwa kutumia kisingizio kwamba bado askari wa Afrika wanaopelekwa nchini Mali katika fremu ya Umoja wa Mataifa hawana utayarifu wa kutosha wa kuchukua nafasi ya vikosi vya Ufaransa, maseneta wa Marekani wameitaka Paris kuendelea kuwepo kijeshi nchini humo hata baada ya mwezi Machi. Seneta Christopher Coons wa chama cha Democrats cha Marekani amedai kwamba, kuimarishwa uthabiti nchini Mali kunahitajia kuwepo kwa muda mrefu askari wa Ufaransa katika nchi hiyo ya Kiafrika. Inasemekana kuwa Maseneta hao katika safari yao hiyo walikutana na kuzungumza na makamanda wa kijeshi wa Mali mjini Bamako. Tarahe 11 Januari Ufaransa ilianza operesheni zake za kijeshi dhidi ya waasi wa kaskazini mwa Mali, na imekuwa ikiungwa mkono kilojistiki na Marekani. Mwezi Januari Marekani ilisisitiza kuwa, msaada wa Washington kwa Ufaransa ungekuwa wa kiushauri na kilojistiki tu na kwamba Marekani haina nia ya kupeleka askari wake nchini Mali. Hivi sasa kuna askari 4,000 wa Ufaransa huko Mali na imepangwa kuwa askari kadhaa kutoka nchi nyingine za Ulaya pia watapelekewa nchini humo kutoa mafunzo kwa wanajeshi wa Mali, ambapo kundi la kwanza la askari hao tayari limewasili mjini Bamako. Umoja wa Ulaya unakusudia kuisaidia Mali yuro milioni 270 ili kufanikisha mipango yake hiyo. Hata hivyo imepangwa kuwa, baada ya kupelekewa nchini Mali askari wote wa kikosi cha nchi wanachama wa Jumuiya ya ECOWAS, askari wa Ufaransa wataanza kuandoka nchini humo. Mashambulizi ya kijeshi ya Paris nchini Mali mbali na kukosolewa na shakshia wa kisiasa wa mirengo ya kulia na kushoto ya Ufaransa pia yamekosolewa na nchi nyingi duniani. Hata hivyo Wafaransa wanadai kwamba, lengo lao la kuingilia kijeshi nchini Mali ni kuimarisha amani na usalama wa nchi hiyo na kuangamiza makundi yenye silaha ya wapinzani. Lakini wataalamu wa mambo wanasema kuwa, umuhimu wa nchi hiyo ya Kiafrika kwa Ufaransa unatokana na maliasili iliyo nayo kama utajiri wa urani, ambayo ina nafasi muhimu katika kudhamini nishati inayohitajika kwenye taasisi za nyuklia za Ufaransa. Vilevile Umoja wa Ulaya umepasisha msaada wa fedha na kupelekwa askari nchini Mali ukiwa na malengo ya kiuchumi na kiusalama kama ya Ufaransa lakini yanayotekelezwa kwa kisingizio cha kupambana na makundi ya kigaidi.  

No comments:

Post a Comment

TUPE MAWAZO YAKO