Thursday, February 28, 2013

SAFARI YA UJUMBE WA IRAN HUKO KAZAKHSTAN


Duru mpya ya mazungumzo kati ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na kundi la 5+1 kuhusu miradi ya nyuklia ya Iran inafanyika leo Jumanne huko Almaty, Kazakhstan. Katibu wa Baraza Kuu la Usalama wa Taifa la Iran Saeed Jalili amewasili Almaty mji mkuu wa Kazakhstan akiongoza ujumbe wa Iran kwa ajili ya kushiriki katika duru hiyo ya mazungumzo. Iran na kundi la 5+1 linaloundwa na Marekani, Russia, Uchina, Ufaransa, Uingereza na Ujerumani mwaka uliopita zilifanya duru tatu za mazungumzo. Duru ya mwisho ya mazungumzo hayo iliyohudhuriwa na Saeed Jalili, Katibu wa Baraza Kuu la Usalama wa Taifa la Iran na Bi Catherine Ashton Mkuu wa Siasa za Nje wa Umoja wa Ulaya ilifanyika mwezi Juni mwaka jana huko Moscow mji mkuu wa Russia.
Wawakilishi wa Majlisi ya Ushauri ya Kiislamu ya Iran yaani bunge wametoa taarifa wakiitaka timu ya mazungumzo ya Iran kutetea kwa nguvu zote haki za taifa la Iran katika fremu ya makubaliano ya kuzuia kuzalisha, kutumia na kusambaza silaha za nyuklia  NPT. Taarifa ya wabunge wa Iran imeashiria pia kushiriki Russia na Uchina katika mazungumzo hayo kama nchi wanachama wa kudumu wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa na kuongeza Iran inataraji kuwa nchi hizo hazitafuata sera za kupenda makuu na matakwa yasiyo na kimantiki ya Marekani bali zitalinda mkataba wa NPT khususan kipengee cha 4 kinachozipa nchi wanachama haki ya kumiliki teknolojia ya nyuklia.
Saeed Jalili Katibu wa Baraza Kuu la Usalama wa Taifa la Iran amesema kabla ya mazungumzo ya Kazakhstan kwamba, wananchi wa Iran wanataka kulindwa haki yao ikiwemo haki ya nyuklia na kwamba Iran kama nchi mwanachama hai na inayofuata sheria, inatekeleza kikamilifu sheria zote katika fremu ya mkataba wa NPT. Matamshi hayo yaliyotolewa kabla ya kuanza mazungumzo ya Almaty yanayonyesha kuwa Iran inaingia katika mazungumzo na kundi la 5+1 katika fremu ya mantiki, inayoeleweka na ya kujilinda huku ikitaraji kuwa muamala wa kundi la 5+1 pia utaegemea katika stratejia iliyo ya wazi.
Inaonekana kuwa duru mpya ya mazungumzo ya nyuklia kati ya Iran na kundi la 5+1 kama kawaida inaanza katika anga ngumu na iliyojaa mashinikizo ya kisiasa. Hii ni katika hali ambayo Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Nyuklia (IAEA) pia umetoa ripoti yake kabla ya kuanza mazungumzo ya leo ukiashiria kufungwa mashinepewa za kisasa katika kiwanda cha Natanz hapa nchini ikiwa ni katika jitihada za wakala huo za kuzusha shaka na wasiwasi kuhusu miradi ya kuzalisha nishati ya nyuklia ya Iran. Hata hivyo aina hiyo ya vita vya kisaikolojia vinavyofanyika sasa  kabla ya kuanza mazungumzo ya leo huko Almaty havina jambo jipya. Moja ya mambo yaliyopelekea kusimamishwa mazungumzo kati ya Iran na kundi la 5+1 kwa karibu miezi tisa ulikuwa  ni muamala  kama huo wa wakala wa IAEA na misimamo yake isiyo ya kimantiki na sera za nchi za Magharibi  mbele ya haki ya kinyuklia ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran. Baadhi ya duru za kisiasa na vyombo vya habari pia vimekuwa vikiukosoa muamala huo wa nchi za Magharibi kuhusiana na Iran.
Kuhusiana na jambo hilo, baadhi ya wanadiplomasia wa nchi za Magharibi wanasema kwamba, Marekani itawasilisha pendekezo jipya katika mazungumzo ya Almaty ili kuhitimisha mkwamo uliosababishwa na  misimamo ya Magharibi katika kadhia ya nyuklia ya Iran. Kwa vyovyote vile, msimamo wa Iran kuhusu mtazamo huo uko wazi na chanya na Tehran inazitaka nchi za Magharibi kutambua rasmi haki yake ya nyuklia ikiwemo urutubishaji wa urani katika fremu ya mkataba wa NPT na si zaidi ya hapo. Iran kwa upande wake itaendelea kuheshimu kikamilifu sheria zote kwa mujibu wa mkataba wa NPT.

No comments:

Post a Comment

TUPE MAWAZO YAKO