Thursday, February 28, 2013

IRAN YAZINDUA MAKOMBORA YA KUTUNGULIA NDEGE


Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu la Iran SEPAH limefanyia majaribio bunduki mpya ya kutungulia ndege ya kubebwa begani na ambayo ina uwezo mkubwa wa kutungua vyombo vya angani hasa helikopta. Hilo limefanyika katika mazoezi ya kijeshi ya jeshi hilo yanayoendelea hivi sasa hapa nchini kwa mfululizo. Msemaji wa luteka hiyo yenye jina la Payambare A'zam 8, Brigedia Jenerali Hamid Sarkheili amesema kuwa, silaha hiyo mpya imebuniwa, kutengenezwa na kuendelezwa na jeshi lenyewe la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu la Iran. 
Ameongeza kuwa, silaha hiyo ina uwezo wa kutungua helikopta iliyoko umbali wa mita 1,400 angani. Jeshi la nchi kavu la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran SEPAH jana Jumamosi lilianza kufanya mazoezi hayo ya kijeshi katika mkoa wa Kerman wa kusini mashariki mwa Iran kwa lengo la kujiimarisha kijeshi na kufanyia majaribio silaha mpya. Jana pia na wakati mazoezi hayo yakiendelea, Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu la Iran kwa mara nyingine lililazimisha kutua chini ndege isiyo na rubani (drone) ya nchi moja ya adui baada ya kuingia kwa siri katika anga ya Iran. Jenerali Sarkheili pia amesisitiza kuwa, kwa kutumia uwezo wake mkubwa wa vita vya kielektroniki, Iran inaweza kuvuruga kwa urahisi mfumo wa makombora ya maadui.

No comments:

Post a Comment

TUPE MAWAZO YAKO