Tuesday, March 26, 2013

CHRISTIAN RONALDO AKATAA KUBADILISHANA JEZI NA MUISRAEL


Christiano Ronaldo nahodha na mshambuliaji machachari wa timu ya taifa ya Ureno na klabu ya Real Madrid ya Uhispania amekataa kubadilishana jezi na mchezaji mwenzake wa utawala wa Kizayuni wa Israel, mara baada ya kumalizika mechi kati ya timu hizo mbili za kuwania tiketi ya kucheza fainali ya kombe la dunia mwaka 2014 nchini Brazil iliyochezwa hivi karibuni huko Tel Aviv, Palestina inayokaliwa kwa mabavu. Takwa la mchezaji wa Israel la kubadilishana jezi na Ronaldo lilikataliwa katika hali ambayo, wachezaji wote waliobakia wa Ureno walikubali kubadilishana jezi na wale wa utawala wa Kizayuni wa Israel. Kitendo cha kubadilishana jezi ni cha kawaida, na hasa kinaonyesha upendo na kinabaki kuwa kumbukumbu kwa wachezaji hao.
Aidha pambano hilo la kundi F, lilimalizika kwa timu hizo mbili kutoshana kwa  sare ya kufungana mabao 3-3. Ureno ilitangulia kupachika bao katika dakika ya 2 lililofungwa na Bruno Alves, na baada ya hapo Israel ilichachamaa na kusawazisha katika dakika ya 40, na kupachika mabao mengine mawili katika dakika za 40 na 70 yaliyofungwa na Ben Basat na Gershon. Ureno nusura iumbuke ugenini, lakini Fabio Coentrao anayechezea Real Madrid ya Uhispania alisawazisha katika dakika za majeruhi 90+3. Ronaldo aliulizwa swali la kichokozi  na lenye mtazamo wa kisiasa na mwandishi mmoja wa habari juu ya suala la nchi ya Israel na kujibu; anachojua yeye ni kwamba amecheza mechi hiyo nchini Palestina, na wala siyo Israel.
Inafaa kuashiria hapa kuwa, mara baada ya utawala wa Kizayuni wa Israel kushambulia eneo la Ukanda wa Gaza mwishoni mwa mwaka 2012, Ronaldo alitoa msaada wa kiasi cha euro milioni moja na nusu kwa ajili ya ukarabati wa shule ilizobomolewa kwa makombora ya ndege za utawala wa Israel. Aidha mwaka 2011 aliwahi kutoa viatu vyake na kupigwa mnada na fedha zilizopatikana alizikabidhi kwa Wapalestina kwa minajili ya kujenga na kukarabati shule za eneo la Ukanda wa Gaza.

No comments:

Post a Comment

TUPE MAWAZO YAKO