Wednesday, March 27, 2013

IRAN YALALAMIKIA MADAU YA SAUDI ARABIA


Iran imemuita balozi mdogo wa Saudi Arabia hapa Tehran na kumkabidhi malalamiko kuhusu madai ya Saudia kuwa Jamhuri ya Kiislamu inafungamana na mtandao wa kijasusi katika ufalme huo wa Kiarabu.
Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran imembainishia mwanadipolmasia huyo wa Saudia malalamiko makali ya Iran kuhusu madai yasiyo na msingi na yanayokaririwa mara kwa mara na Saudia. Iran aidha imeitaka Saudi Arabia itoe maelezo rasmi kuhusu kadhia hiyo. Balozi wa Saudi Arabia nchini Iran hakuwepo na hivyo balozi mdogo ndiye aliyekabidhiwa malalamiko yao.
Wakati huo huo wanazuoni kadhaa wa Kiislamu nchini Saudi Arabia wameutaka utawala wa Riyadh kuwaachilia huru watu 18 waliotiwa mbaroni kwa madai ya kuwa na uhusiano na Iran. Watu hao 18 wamekanusha tuhuma dhidi yao na kusema utawala wa Saudia unajaribu kupotosha fikra za umma kuhusu matakwa ya wananchi wanaotaka marekebisho nchini humo. Kuna karibu wafungwa 30 elfu wa kisiasa kote Saudia ambao wanashikiliwa pasina kufunguliwa mashtaka au baada ya muhula wa vifungo vyao kumalizika.

No comments:

Post a Comment

TUPE MAWAZO YAKO