Thursday, March 28, 2013

KIONGOZI WA WAASI WA JAMHURI YA KATI AJIPANGA KUTANGAZA SERIKALI YAKE


Kiongozi wa Waasi wa Kundi la Seleka ambaye amejitangaza Rais wa Jamhuri ya Afrika ya Kati, Michel Djotodia anatarajiwa kutangaza serikali yake ambayo ameahidi itakaa madarakani kwa kipindi cha miaka mitatu kabla ya kuitisha uchaguzi mkuu. Serikali hiyo mpya inatarajiwa kushika nafasi ya ile iliyoangushwa ya Rais Francois Bozize ili kuongoza nchi hiyo ambayo imetengwa na Umoja wa Afrika AU pamoja na Umoja wa Mataifa UN ambao umelaani mapinduzi hayo. Djotodia amesema kuwa Serikali atakayoiunda itakuwa na jukumu la kuhakikisha inaimarisha usalama wa nchi hiyo pamoja na kuleta utangamano miongoni mwa wananchi ambao walikuwa wamegawanyika wakati wa utawala wa Bozize.
Kiongozi huyo ameongeza kuwa wakati huu ambapo aiunda Serikali, ameunda kikosi maalumu cha askari ambacho kitakuwa na jukumu la kuhakikisha kinawashughulikia wale wote ambao wanadaiwa kushiriki katika vitendo vya uvunjifu a amani ambapo wakati wanaingia kwenye mji huo wanajeshi wa Seleka waliripotiwa kupora mali. Jumuiya ya kimataifa imelaani matukio ambayo yamekuwa yakifanywa na wanajeshi wa Seleka wanaodaiwa kushiriki vitendo vya uvunjifu wa amani kwa kuwanyanyasa raia pamoja na kuwalazimisha kuchukua mali zao kwa nguvu.
Hali ya machafuko imesababisha madhara makubwa kwa vijana na hata wengine kujikuta wakiingia kwenye vitendo vya uporaji nchini Jamhuri ya Afrika ya Kati jambo ambalo limeainishwa pia na shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulika na watoto UNICEF. Serikali ya Seleka imekumbana na ukosoaji mkubwa kutokana na kuiangusha serikali halali huku Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa UNSC likiahidi kuchukua hatua madhubuti dhidi yao.

No comments:

Post a Comment

TUPE MAWAZO YAKO