Saturday, March 30, 2013

MAITI ZAPATIKANA MJI WA BANGUI

Shirika la Msalaba Mwekundu la Jamhuri ya Afrika ya Kati limetangaza kuwa, makumi ya maiti zimepatikana katika mji mkuu wa nchi hiyo Bangui tangu waasi wa Seleka walipoipindua serikali ya Francois Bozize mwishoni mwa juma lililopita. Albert Yomba Eyamo, afisa wa Shirika la Mlasaba Mwekundu katika Jamhuri ya Afrika ya Kati amewaambia waandishi wa habari kwamba, hadi sasa wafanyakazi wa shirika hilo wameokota maiti 78 katika mitaa na barabara za mji mkuu Bangui na kuzihamishia katika vyumba vya kuhifadhia maiti. Habari ya kupatikana maiti hizo imetangazwa sambamba na maadhimisho ya sherehe za kitaifa za kujipatia uhuru nchi hiyo kutoka kwa mkoloni Mfaransa. Wakati huo huo habari kutoka mji mkuu Bangui zinasema kuwa, hali ya kimaisha katika mji huo ni mbaya huku baadhi ya maeneo yakiwa hayana maji wala umeme. Ikumbukwe kuwa, tarehe 24 ya mwezi huu wa Machi, muungano wa waasi wa Seleka uliyadhibiti maeneo nyeti ya Jamhuri ya Afrika ya Kati ikiwemo ikulu ya Rais hali iliyomlazimisha Rais Francois Bozize wa nchi hiyo aikimbie nchi. Bozize kwa sasa yuko nchini Benin baada ya kuondoka Kongo na Cameron.

No comments:

Post a Comment

TUPE MAWAZO YAKO