Wednesday, March 27, 2013

MISIKITI NA NYUMBA KADHAA ZA WAISLAM ZACHOMWA MOTO MYANMAR


Misikti miwili na nyumba kadhaa za Waislamu zimeteketezwa kwa moto katika mashambulizi mapya dhidi ya Waislamu wa kabila la Rohingya nchini Myanmar. Afisa wa polisi ambaye hakutaka jina lake litajwe amesema kuwa mashambulizi hayo yametokea katika vijiji vya eneo la Bago kaskazini mwa mji wa Yangon siku ya Jumatatu.
Amesema hakuna habari zozote kuhusu mauaji katika mashambulizi ya hivi karibuni dhidi ya Waislamu walio wachache katika nchi hiyo ya kusini mashariki mwa Asia.
Mnamo Machi 20 Mabuddha wenye misimamo mikali waliteketeza kwa moto nyumba za Waislamu na misikiti katika mji wa Meiktila nchini Myanmar ambapo watu 40 waliuawa na wengine 12,000 kuachwa bila makao. Wakati huo huo mshauri wa Umoja wa Mataifa kuhusu Myanmar, Vijay Nambiar, ameitaka serikali ya nchi hiyo kuwaadhibu wanaofanya mashambulizi dhidi ya Waislamu.
Inafaa kukumbusha hapa kuwa, serikali ya Myanmar inawabagua, inawatesa na kuwakandamiza Waislamu wa Rohingya ambao idadi yao inafikia laki nane kwa madai kwamba, Waislamu hao ni wakimbizi waliokimbilia nchini humo wakitokea nchini Bangladesh.

No comments:

Post a Comment

TUPE MAWAZO YAKO