Thursday, March 28, 2013

VIONGOZI WA KIISLAM MYANMAR WAMLILIA RAIS WAO

Viongozi wa Kiislamu nchini Myanmar wamemuomba Rais Thein Sein kuchukua hatua za haraka kukomesha vurugu, wakivituhumu vyombo vya usalama kwa kuangalia tu wakati waandamanaji wakifanya ghasia. Katika barua ya wazi waliyoituma kwa Rais Thein, makundi manne yakiwemo Baraza la Masuala ya Dini ya Kiislamu na Shirika la Kitaifa la Masuala ya Waislamu, yamesema mashambulizi hayo yanahusisha uhalifu kama vile uchomaji moto na mauaji, ambayo yanastahili adhabu kali, lakini mamlaka zilishindwa kuwachukulia hatua wahalifu ambao wametenda makosa hayo mbele ya macho yao. Watu wasiopungua 40 wameuawa na misikiti kuchomwa katika miji kadhaa katikati mwa Myanmar, tangu kuibuka kwa vurugu mpya za kidini tarehe 20 Machi. Machafuko ya sasa yalisababishwa na mzozo katika duka la kuuza dhahabu, na kugeuka ghasia ambapo misikiti na nyumba vilichomwa, huku miili ya watu iliyoungua ikizagaa barabarani. Lakini mashahidi wanasema vurugu hizo zinaonekana zilipangwa.

No comments:

Post a Comment

TUPE MAWAZO YAKO