Thursday, March 28, 2013

WAKOREA KUSINI WARUHISIWA KUINGIA KASKAZINI


Raia wa Korea Kusini wameruhusiwa kusafiri kwenda katika eneo la viwanda linalonedeshwa kwa pamoja nchini Korea Kaskazini, licha ya utawala mjini Pyongyang, kukata mawasiliano ya simu ya kijeshi ya mpakani siku ya Jumatano. Msemaji wa wizara ya muungano ya Korea Kusini amesema karibu watu 400 kutoka Korea Kusini walivuka mpaka pasipo kuchelewesha asubuhi ya leo.
Korea Kaskazini ilikata mawasiliano ya simu inayotumika kuratibu usafiri kwenda na kutoka eneo la viwanda la Kaesong, ambalo ni moja ya vyanzo vya mapato ya kigeni kwa taifa hilo lenye kiwango kikubwa cha umaskini. Karibu kampuni 120 za Korea Kusini zinaendesha shughuli zake katika eneo la Kaesong, na zinaajiri pia wafanyakazi wa Korea Kaskazini. Korea Kaskazini ilisema siku ya Jumatano kuwa ilikuwa inakata mawasiliano hayo, kutokana na tabia za kiuadui kutoka kwa Marekani na Korea Kusini, ambazo zilifanya mazoezi ya kijeshi mwezi huu.

No comments:

Post a Comment

TUPE MAWAZO YAKO