Sunday, March 31, 2013

WANAOGOMBEA KITI CHA URAIS IRAN WAONGEZEKA


Waziri wa Barabara na Ustawi wa Miji Iran Ali Nikzad ametangaza rasmi uamuzi wake wa kugombea kiti cha urais katika uchaguzi ujao nchini na hivyo kufanya idadi ya waliotangaza azma ya kugombea kiti hicho kuwa tisa. Nikzad alitangaza uamuzi wake huo Jumamosi alipotembelea mji wa Ardebil ulio kaskazini magharibi mwa Tehran.
Uchaguzi wa 11 wa rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran utafanyika mwezi Juni na wagombea wote wanatakiwa kujiandikisha kati ya Mei 7 na 11. Rais Mahmoud Ahmadinejad anamaliza muhula wake wa pili na hivyo kikatiba hawezi kugombea. Kati ya waliotangaza kuwa tayari kugombea kiti cha urais Iran ni pamoja na waziri wa zamani wa mambo ya nje Manouchehr Mottaki, manaibu spika wawili wa bunge Sheikh Mohammad Hassan Aboutorabi-Fard na Mohammad Reza Bahonar. Wengine waliotangaza nia ya kuwania urais wa Iran ni pamoja na waziri wa zamano wa mambo ya ndani Sheikh Mostafa Pour-Mohammadi, mwanachama mwandamizi wa Halmashauri ya Kuainisha Maslahi ya Mfumo, Sheikh Hassan Rohani, Halmashauri ya Kuainisha Maslahi ya Mfumo Dkt. Mohsen Rezaei, waziri wa zamani wa usalama wa ndani Sheikh Minister Ali Fallahian na waziri wa zamani wa nyumba Mohammad Saeedi-Kia. Rais wa Iran huchaguliwa baada ya miaka minne na wagombea wote huidhinishwa baada ya kuchunguzwa na Baraza la Kulinda Katiba.

No comments:

Post a Comment

TUPE MAWAZO YAKO