Sunday, April 21, 2013

CHINA YAILAUMU MAREKANI KUHUSU HAKI ZA BINADAMU

Serikali ya China imeilaumu vikali Marekani kwa kufumbia macho uvunjaji mkubwa wa haki za binadamu unaofanywa na nchi hiyo katika kila kona ya dunia na badala yake Washington inazituhumu nchi nyingine kukanyaga haki hizo. Taarifa ya Baraza la Mawaziri la China iliyotolewa leo imeongeza kuwa, Marekani imekuwa ikivunja wazi wazi haki za binaadamu kwenye operesheni zake za kijeshi katika kona mbalimbali za dunia na kwa hatua yake ya kuyasaidia kifedha makundi ya waasi ambayo yanavuruga misingi ya kidemokrasia katika nchi mbalimbali duniani. Katika ripoti yake iliyoipa jina "Rekodi ya Haki za Binaadamu Nchini Marekani Mwaka 2012," China imesema pia kuwa, machafuko ya kutumia silaha moto nchini Marekani ni mfano mwingine wa uvunjwaji wa haki za binadamu nchini humo. Imesema, mashambulizi ya kiholela ya kutumia silaha moto yameendelea kuwa tishio kubwa kwa usalama na maisha ya wananchi wa kawaida nchini Marekani. Lawama hizo dhidi ya Marekani zimekuja katika hali ambayo Baraza la Haki za Binaadamu la Umoja wa Mataifa nalo limeilaumu nchi hiyo kutokana na mashambulizi ya ndege zake za kigaidi zisizo na rubani zinazoua watu wa kawaida katika nchi mbali ulimwenguni.

No comments:

Post a Comment

TUPE MAWAZO YAKO