Tuesday, April 23, 2013

RAIS MUSEVEN ABEBA PESA KWENYE VIROBA


Rais wa Uganda Yoweri Museveni amebuni mbinu mpya ya kuyasaidia Makundi ya vijana nchini mwake kwa kuwakabidhi fedha hizo moja kwa moja kwa lengo la kuepukana na ufisadi ambao umeota mizizi na kuchangia misaada yake kushindwa kuwafikia walengwa. Jumatatu hii Rais Museveni alikabidhi pesa taslimu zipatazo shilingi milioni 25 za Uganda sawa na dola za Marekani laki moja kwa kikundi cha vijana wa Busoga, fedha hizo ziliwasilishwa zikiwa katika gunia suala ambalo limezua hisia mbalimbali kwa wananchi wa Taifa hilo.
Televisheni ta Taifa ya nchi hiyo NTV, ilimuonyesha Rais Museveni akikabidhi fedha hizo, misaada mingine aliyokabidhi kwa vijana wa kikundi hicho cha Busoga Youth Forum ni pamoja na basi dogo, lori na pikipiki 15 ambazo ni ahadi alizozitoa katika kampeni zake za uchaguzi mkuu wa mwaka 2011. Wanaharakati wa kupambana na rushwa na vyama vya upinzani nchini humo wamekosoa hatua ya Rais Museveni kutumia njia hiyo kama mbinu ya kuepukana na suala la ufisadi.
Aidha wakosoaji hao wamesema suala la kupambana na umasikini kwa vijana lilipaswa kuratibiwa na Ofisi ya Rais kwa kufuata taratibu maalumu za serikali na sio Rais kutumia njia hiyo ambayo huenda ikasababisha fedha hizo kutumiwa tofauti na malengo yaliyokusudiwa.

No comments:

Post a Comment

TUPE MAWAZO YAKO