Tuesday, April 09, 2013

UFARANSA YAANZISHA OPERESHENI MPYA NCHINI MALI

Majeshi ya Ufaransa yameanzisha duru mpya ya mashambulio makubwa ya kijeshi kaskazini mwa Mali. Takribani wanajeshi elfu moja wa Ufaransa wanashiriki katika operesheni hiyo inayolenga kambi na ngome za makundi ya waasi kwenye viunga vya mji wa Gao ulioko kaskazini mashariki mwa Mali. Jenerali Bernard Barrera kamanda wa kikosi cha ardhini cha majeshi ya Ufaransa yaliyoko Mali amewaambia wanahabari kwamba, operesheni hiyo inajumuisha madazeni ya magari ya kijeshi, helikopta, ndege za kijeshi, ndege zisizo na rubani pamoja na zana nzito za kijeshi. Mji wa Gao ni ngome ya makundi ya watu wanaobeba silaha ambao wanaendesha mapambano dhidi ya serikali ya mpito ya Mali kama vile Harakati ya Jihadi na Uadilifu Magharibi mwa Afrika ambayo hadi vikosi vya Ufaransa vinaingia Mali, ilikuwa inayadhibiti maeneo ya kaskazini mwa nchi hiyo. Baada ya kuanza mashambulio ya Ufaransa, hivi sasa makundi ya waasi yanajikusanya upya ili kuiondoa miji kama Gao, Kidali na Timbuktu kutoka katika udhibiti wa jeshi la Mali na lile la Ufaransa. Upinzani mkali wa makundi ya waasi ya Mali dhidi ya uingiliali wa kijeshi wa vikosi vya Ufaransa nchini humo umeshuhudiwa zaidi katika mji wa Gao. Mapigano katika mji wa Gao na wasi wasi wa kutokea mauaji ya ulipizaji kisasi ni jambo linalotajwa na weledi wa mambo kuwa, limekuwa na nafasi muhimu ya kukithiri raia wa nchi hiyo wanaokimbia makazi yao na kuomba hifadhi katika nchi jirani na Mali. Wakimbizi wa Mali waliokimbilia kwenye katika maeneo ya mpakani na Niger wana upungufu mkubwa wa chakula, ukosefu wa amani huku na umasikini mkubwa. Hivi sasa maelfu ya raia wa kabila la Tuareg wamevuka Mto Niger na kuomba hifadhi kaskazini mwa mto huo wakihofia wimbi jipya la mashambulio. Hata wakimbizi walioko kwenye mipaka ya mashariki mwa Mali nao wamelazimika kukimbilia katika nchi za Mauritania na Burkina Faso. Kamanda wa majeshi ya Ufaransa nchini Mali anadai kwamba, makundi ya wabeba silaha katika maeneo ya milima ya Ifoghas yameshindwa na yamelazimika kurejea nyuma.  Kwa mujibu wa Jenerali Bernard Barrera, majeshi ya Ufaransa sasa yameelekeza nguvu na operesheni zake za kijeshi katika viunga vya katikati mwa Mali. Laurent Fabius, Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Ufaransa ambaye hivi karibuni alitembelea mji mkuu wa Mali, Bamako, ametoa pendekezo kwa Umoja wa Mataifa na serikali ya mpito ya Mali la kubakia daima askari 1000 wa Ufaransa katika nchi hiyo ya magharibi mwa Afrika. Wachambuzi wa mambo wanaamini kuwa, hatua ya Ufaransa ya kutuma majeshi yake kaskazini mwa Mali haikuchukuliwa na nia njema na ya dhati ya moyo ya kupambana na makundi ya waasi, bali ni kwa tamaa na uchu wa kupora utajiri wa madini ya urani, dhahabu na almasi wa nchi hiyo.

No comments:

Post a Comment

TUPE MAWAZO YAKO