Tuesday, April 02, 2013

MSHAURI WA WAZIRI MKUU WA LIBYA ATEKWA NYARA


Duru za habari zimeripoti kwamba mshauri wa Waziri Mkuu wa Libya ametekwa nyara. Mfanyakazi mmoja wa ofisi ya Waziri Mkuu wa Libya amefichua kuwa Muhammad Ali Al Qatus ambaye ni Mshauri wa Waziri Mkuu wa Libya, Ali Zaidan ametekwa nyara na gari lake limepatikana katika mtaa wa Tajura katika viunga vya mji wa Tripoli. Tukio hilo limetokea baada ya Waziri Mkuu wa Libya mwenyewe na baadhi ya mawaziri wa serikali yake kutishiwa kifo. Ishara zinaonesha kuwa hali ya usalama nchini Libya imeingia katika awamu mpya na tata hususan baada ya kuanza mashambulizi ya waasi dhidi ya viongozi na taasisi za serikali ya Tripoli.
Vyombo rasmi vya habari vya Libya wiki iliyopita pia viliripoti kuwa maafisa kadhaa wa polisi wa jiji la Tripoli walikuwa wametekwa nyara na kundi la wanamgambo na wafuasi wa makundi yenye misimamo mikali. Maafisa wa Wizara ya Mambo ya Ndani pia walikuwa miongoni ma waliotekwa nyara na kundi hilo. Ingawa Tripoli ilikanusha habari hiyo lakini baadhi ya maafisa wa Congresi ya Taifa la Libya walithibitisha kuwa makundi ya waasi yameanzisha wimbi la mauaji ya kigaidi na kuwateka nyara askari wa serikali. Siku chache zilizopita makundi ya wanamgambo ya Libya yalivamia ofisi ya Waziri Mkuu wa nchi hiyo mjini Tripoli na Jumapili iliyopita wafuasi wa makundi hayo walishambulia jengo la Wizara ya Sheria.
Mwenyekiti wa Kamati Kuu ya Usalama ya Tripoli Hashim Bashir anasema kuwa shambulizi hilo lilifanyika baada ya Waziri wa Sheria Salah Mirghani kutangaza kuwa, si halali kwa makundi ya wanamapinduzi kudhibiti baadhi ya jela za Tripoli. Baadhi ya jela na magereza za miji ya Tripoli, Misrata, Zawira na Jabal al Gharbi zingali zinadhibitiwa na makundi ya wafanyamapinduzi wa Libya licha ya kuundwa serikali ya mpito nchini humo. Mbali na jela miji kadhaa ya nchi hiyo pia inadhibitiwa ama na makundi ya wanamgambo walioshiriki kwenye mapinduzi ya Libya au wafuasi wa utawala uliong'olewa madarakani wa Muammar Gaddafi. Kwani hadi sasa viongozi wa serikali ya Libya hawajafanikiwa kudhibiti maeneo yote ya nchi hiyo. Suala hilo pamoja na vita vya kugombea madaraka baina ya makabila ya Libya kwa upande mmoja na baina ya serikali na wanamapinduzi wa zamani kwa upande mwingine vinaitumbukiza nchi hiyo katika lindi la ukosefu wa amani.
Majaribio ya kutaka kuuawa viongozi wa ngazi mbalimbali na serikali na jeshi la Libya yamekuwa yakifanyika karibu kila siku. Jaribio la hivi karibuni lilimlenga Kanali Waniis Bu Khmadah, kamanda wa jeshi la Libya kusini mwa nchi hiyo. Kanali Bu Khmadah aliokoka jaribio hilo. Katika kipindi cha mwaka mmoja uliopita maeneo ya kusini mwa Libya ikiwamo miji ya Sabha na al Kafara yamekuwa yakikumbwa na mashambulizi ya makundi ya kigaidi. Maafisa wa serikali ya Libya wanayahusisha mashambulizi hayo na wapiganaji kutoka Chad wanaoingia nchini humo au mapigano yanayojiri kati ya makabila ya Kiarabu na Kiafrika  kusini mwa Libya. Hapana shaka kuwa kuendelea hali hii ya ukosefu wa amani nchini Libya kunatishia mapinduzi ya wananchi na kufungua mlango wa madola ya kibeberu kuingia zaidi mambo ya ndani ya nchi hiyo. Hususan ikitiliwa maanani kwamba baadhi ya nchi za Magharibi zinakodolea macho kwa uroho maliasili na utajiri wa mafuta na gesi wa Libya.

No comments:

Post a Comment

TUPE MAWAZO YAKO