Rais Jacob Zuma wa Afrika Kusini amesema kuwa, nchi yake itaondoa vikosi vyake vya kijeshi huko katika Jamhuri ya Afrika ya Kati. Kauli ya Zuma imekuja masaa machache tu baada ya Xolani Mabanga Msemaji wa jeshi la Afrika Kusini kutoa kauli kama hiyo. Rais Zuma amesema, Pretoria imefikia uamuzi wa kuondoa vikosi vyake huko Jamhuri ya Afrika ya Kati kwani jukumu la vikosi hivyo lilikuwa ni kusaidia kutoa mafunzo kwa vikosi vya serikali ya Rais Francois Bozize na kwamba, baada ya serikali yake kupinduliwa na waasi hakuna serikali katika nchi hiyo. Zuma ametoa tangazo hilo huku wanajeshi 13 wa nchi hiyo wakiwa wameuawa huko Jamhuri ya Afrika ya Kati na wengine 27 kujeruhiwa baada ya kujiri mapigano kati yao na waasi wa Seleka Machi 23 katika kituo cha upekuzi mjini Bangui. Januari mwaka huu Afrika Kusini ilituma kikosi cha wanajeshi 200 katika Jamhuri ya Afrika ya Kati kwa lengo la kuisaidia serikali ya Bozize katika kukabiliana na waasi. Wakati huo huo, Waziri wa Ulinzi wa Afrika Kusini amesema kuwa, nchi yake haijatoa ahadi ya kutoa hifadhi kwa Francois Bozize Rais wa Jamhuri ya Afrika ya Kati aliyepinduliwa madarakani.
No comments:
Post a Comment
TUPE MAWAZO YAKO