Friday, May 24, 2013

AU YATAKA KESI YA VIONGOZI WA KENYA IFUTWE


Nchi za Afrika zimeunga mkono ombi la Kenya la kutaka kesi ya jinai dhidi ya rais wake kufutwa katika mahakama ya Kimataifa ya Jinai ICC. Duru za kidiplomasia zinasema Umoja wa Afrika umeafiki ombi la Kenya la kutaka kesi dhidi ya Rais Uhuru Kenyatta na naibu wake William Ruto iondolewe ICC na badala yake kusikilizwa nchini Kenya. Pendekezo hilo la Kenya lilijadiliwa katika kikao cha Mawaziri wa Mambo ya Nje wa Umoja wa Afrika waliokutana Alkhamisi huko Addis Ababa Ethiopia. Pendekezo hilo linatazamiwa kuidhinishwa katika mkutano wa kilele wa viongozi wa AU ambao watakutana kesho katika mji mkuu huo wa Ethiopia. Serikali ya Kenya imesema kesi za ICC dhidi ya viongozi wake zitahatarisha usalama wa nchi hiyo yenye uchumi mkubwa zaidi mashariki mwa Afrika.
Wakati huo huo Nafie Ali Nafie Mshauri wa Rais Omar el Bashir wa Sudan amesema huenda nchi za Afrika kwa pamoja zikapitisha azimio la kujiondoa ICC. Ikumbukwe ICC imetoa waranti wa kutiwa mbaroni Rais Bashir wa Sudan. Kwingineko Rais Salva Kiir wa Sudan Kusini amesema nchi yake inapinga kesi ya ICC dhidi ya Rais Uhuru Kenytta. Ameyasema hayo baada ya kukutana na Kenyatta mjini Juba siku ya Alkhamisi. ICC inalaumiwa kuwa ina muelekeo wa kisiasa katika kesi zake ambazo zote zinalenga nchi za Afrika.

No comments:

Post a Comment

TUPE MAWAZO YAKO