Sunday, May 26, 2013

JESHI LA UFARANSA LAANZA KUONDOA ZANA ZAKE MALI

Msafara wa malori makubwa umeondoka katika kambi ya Wafaransa karibu na mji mkuu, Bamako, kuelekea kusini katika nchi ya jirani, Ivory Coast. Ufaransa ilituma wanajeshi 4,500 nchini Mali mwezi wa Januari kwenda kupambana na wapiganaji wa Kiislamu. Inapanga kukabidhi jukumu hilo kwa jeshi la Mali na kikosi cha Umoja wa Mataifa mwezi Julai.
Wanajeshi wa Ufaransa walipoingia Mali walishangiliwa sana. Wananchi wengi wa Mali wanaogopa wanajeshi hao kuondoka. Msafara ulioondoka Bamako ni mkubwa, lakini Wafaransa wanasisitiza kuwa kwa sasa wanaondosha zana na malori ambayo hayahitajiki. Kwa sasa vifaru na magari makubwa ya deraya yatabaki kaskazini mwa Mali. Ufaransa bado ina wanajeshi 3,800 katika koloni yake hiyo ya zamani.
Inasema itapunguza idadi hadi 2,000 mwezi Septemba, na watabaki 1,000 tu ufikapo mwisho wa mwaka.
Shughuli za kuhama zimeanza siku mbili tu baada ya wapiganaji wa Kiislamu kulenga mgodi wa uranium katika nchi jirani na Mali, yaani Niger. Haijulikani shambulio litaathiri vipi matumizi ya jeshi la Ufaransa katika kanda hiyo ya Afrika Magharibi.

No comments:

Post a Comment

TUPE MAWAZO YAKO