Friday, May 24, 2013

WAASI WA MALI WADAI KUWA WALISHAMBULIA NIGER

Kundi moja la waasi wa Mali linalojulikana kwa jina la Harakati ya Tawhid na Jihadi ya Afrika Magharibi (MUJAO) limedai kuwa ndilo lililohusika na miripuko miliwi ya magari yaliyokuwa yametegwa mabomu katika nchi jirani ya Niger na kupelekea zaidi ya watu 20 kuuawa. Msemaji wa kundi hilo, Abu Walid Sahraoui amesema kuwa, kundi hilo lilifanya shambulizi hilo jana Alkhamisi ili kuliadhibu njeshi la Niger kwa kushirikiana na mkoloni wa Ulaya, Ufaransa kuvamia na kufanya mauaji nchini Mali. Miripuko hiyo imetokea kwenye kambi moja ya jeshi na katika mgodi mmoja wa urani katika miji ya Agadez na Artil huko kaskazini magharibi mwa Niger na kupelekea watu wasiopungua 26 kuuawa 20 kati yao wakiwa ni wanajeshi. Mashambulizi ya namna hiyo ni ya kwanza kutokea nchini Niger tangu nchi hiyo ilipoamua kushirikiana na Ufansa katika vita dhidi ya waasi nchini Mali. Ufaransa ambayo ni mkoloni mkongwe wa Ulaya huko magharibi mwa Afrika, iliivamia Mali tarehe 11 Januari mwaka huu kwa madai ya kupambana na waasi, uvamizi ambao umesababisha mgogoro mkubwa wa kibinaadamu katika maeneo ya kaskazini mwa Mali huku maafisa wa kijeshi wa Mali wakiilaumu Ufaransa kuwa ilikuwa na nia ya kujizatiti kijeshi tu katika eneo hilo na si kumaliza uasi. Hadi leo Ufaransa imekataa kuondoka kwenye eneo hilo lenye utajiri mkubwa wa maliasili kwa madai kuwa waasi bado wana ushawishi kwenye maeneo hayo.

No comments:

Post a Comment

TUPE MAWAZO YAKO