Saturday, May 25, 2013

WAISLAM WA MYANMAR WAWEKEWA KIKOMO CHA KUZAA


Wakuu wa jimbo la Magharibi nchini Myanmar wamepitisha sheria inayopiga marufuku familia za Waislamu wa kabila la Rohingya kuzaa watoto zaidi ya wawili. Kwa kutumia kisingizio cha kupunguza mivutano kati ya Waislamu na Mabudha ambayo imesababisha machafuko na mashambulio makubwa na ya kikatili dhidi ya jamii ya wachache ya Waislamu wa Myanmar, wakuu wa jimbo la Rakhin wamepitisha sheria inayowataka Waislamu wasiwe na watoto zaidi ya wawili. Duru za habari zimemnukuu afisa mmoja wa jimbo hilo akisema kuwa sheria hiyo itahusisha miji miwili iliyoko kwenye mpaka wa pamoja wa Myanmar na Bangladesh na ambayo ndiyo yenye idadi kubwa zaidi ya Waislamu. Wein Maying, msemaji wa serikali ya jimbo la Rakhin ametangaza kuwa sheria hiyo ilipitishwa wiki mbili zilizopita baada ya tume iliyoundwa na serikali kupendekeza ianzishwe sera ya uzazi wa mpangilio ili kupunguza mivutano katika eneo hilo lenye mgogoro.
Mashambulio na vitendo vya kikatili dhidi ya Waislamu nchini Myanmar vilianza tangu mwaka mmoja nyuma ambapo Mabudha wenye silaha baridi wamezishambulia nyumba za Waislamu na kuwaua kwa halaiki mamia miongoni mwao na kuwafanya wengine zaidi ya laki moja kuwa wakimbizi baada ya kubaki bila makaazi. Serikali ya Myanmar haiwatambui Waislamu wa kabila la Rohingya kuwa ni raia wa nchi hiyo bali inadai kwamba ni wahajiri wa Kibangladeshi. Hii ni katika hali ambayo kwa mujibu wa Umoja wa Mataifa Waislamu wa kabila la Rohingya ni moja ya jamii za wachache duniani wanaonyongeshwa na kukabiliwa na manyanyaso na mateso makubwa

No comments:

Post a Comment

TUPE MAWAZO YAKO